Friday, July 27, 2012

TAIFA WAENDELEE KUWAKUMBUKA MASHUJAA WA NCHI


Jumatano iliyopita kwenye viwanja vya mnazi mmoja hapa jijini Dar es
Salaam Watanzania tuliadhimisha sikukuu ya mashujaa.Ni siku adimu
katika nchi yetu inayowakumbuka  wazalendo wenzetu waliojitoa mhanga
kutumikia na kuitetea Tanzania dhidi ya wakandamizaji na waporaji
raslimali zetu  kwa manufaa yao



Taifa lolote lililo hai  lazima liishi huku likiendelea kuandika
historia yake. Sina hakika kama Tanzania ina rekodi ya kuwatambua
mashujaa wake na kutunza kumbukumbu zao ili vizazi vingine vijifunze
uzalendo wa vizazi vilivyowatangulia kuon jinsi walivyoweza kuipigania
kwa nguvu na moyo  wote kwa manufaa yetu

Tafsiri ya shujaa ni pana kuliko tunavyodhani, aghalabu  tunadhani
askari na makamanda wao waliopigana vita mbalimbali ndio mashujaa
tunaopaswa kuwakumbuka.Lakini Darubini inaona kuwa orodha ya mashujaa
ni ndefu na wamezagaa kila mahali huenda unahitajika  utafiti wa
kutosha ili kuwatambua

Mara nyingi askari majeshini ya ulinzi na usalama, kutunukiwa nishani
ya utumishi uliotukuka na wa muda mrefu na pia nidhamu na Mheshimiwa
Rais (Amiri Jeshi Mkuu)  lengo ni  kuhamisisha askari kuwa tayari
kuilinda nchi yao  na wao kuingia kwenye rekodi hiyo na hatimaye kuwa
mashujaa wa nchi yetu

Huu ni  utaratibu unaostahili kupongeza tumeona serikali ya awamu ya
kwanza kuwaenzi mashujaa wake hasa maaskari waliopoteza maisha yao
wakitetea nchi yetu na bara la Afrika kwa makuburi yao kutunzwa na
kujengewa minara ya kumbukumbu za mashujaa hao na utamaduni huu
ulienea karibu kila mkoa

Mashujaa si askari pekee yao, wapo mashujaa wengi waliojitolea maisha
yao kwa ajili ya watanzania Lakini kwa vile hatuna chombo cha kitaifa
cha kuwatambua mashujaa hawa vifo na kumbukumbu zao huwa vifo fofofo.
Hii ni dhulma na deni kubwatunalodaiwa na  kama taifa tunapaswa sasa
kuiondoa

Dhana ya sikukuu ya mashujaa  na sherehe mbalimbali zinazofanyika kama
vile  siku ya  utumishi wa umma, kuadhimisha mafanikio ya kila mwaka
ya mashirika na kampuni umma na binafsi nazo hazioneshi kuchochea
hamasa ya uzalendo  na ili  kuwapata mashujaa waliotoa mchango mkubwa
kwa manufaa  umma

Kuwepo wa chombo maalum kitakachoweza kufuatilia na kutawangaza
wanaostahili kuwa mashujaa, kitahamasisha wananchi wengi kupagawa na
kujenga moyo wa uzalendo wa kutumia akili zao na ubunifu kuijenga na
kuilinda Tanzania. Isitoshe kila mara tutakuwa tunazalisha mashujaa
kizazi hadi kizazi

Kwa sasa siku ya mashujaa tunaiona ni siku ya kuweka ngao na mishale
kwenye minara Sikukuu yenyewe  hailengi  kutimiza kile
kinachokusudiwa. Utamaduni wa kuwatambua mashujaa haueleweki. Namna ya
kuwatunza wakiwa hai hata maziko yao hayana utaratibu Hali hii
inachangia kuvunjika kwa moyo wa kujituma


Kukosekana kwa chombo na vigezo vya kuwapata mashujaa kumesababisha
wapewao  tuzo za ushujaa  matajiri, viongozi waandamizi serikalini  na
familia zao na hata wajanja janja hasa mijini. Kama taifa hajaweka
misingi ya kuwatambua maelfu ya mashujaa waliofanya kazi kwa uadilifu
mkubwa tena katika mazingira magumu na muda mrefu ili waorodheshwe
kama mashujaa

Utoaji tuzo za ushujaa sasa umekuwa kama mchezo wa kuigiza na wakati
mwingine unapangwa kati ya mtoaji tuzo na mpokeaji. Haiwezekani mtu
anaingia kazini leo, anapata cheo kesho na kesho kutwa anatangazwa ni
shujaa au anatoa msaada leo halafu kesho anatangazwa ni shujaa
aliyejitoa mhanga

Kama ilivyodhamiria Serikali ya awamu ya nne wakati ikiingia
madarakani kuwa imepania  kufufua  moyo wa uzalendo. Ikiwa inataka
kweli kufufua uzalendo ni lazima ihakikishe kuna utaratibu wa kitaifa
wa kuwatambua na kuwatuza wale walitoa mchango mkubwa kwa kipimo
kinachokubalika  kwa sasa na baadaye.

Tusipokuwa na utaratibu unaoeleweka,  ushujaa wa mtu unaweza kuwa ni
urithi kwenye  familia zenye majina yaliyojengwa kutokana na dhamana
za kitaifa au wale wanaonunua umaarufu . Piaa tukiadhimisha siku ya
mashujaa kwa mazoea kama ilivyokuwa huko nyuma dhana ya ushujaa nayo
itapotea muda mfupi ujao

Kuna watumishi wa serikali, wanasayansi, wachumi, waalimu  wasanii na
wengineo wengi wametoa michango mikubwa na kwamba  kungekuwepo na
mchakato unaotambulika wangeingizwa kwenye orodha ya mashujaa wetu na
kuwa miongoni  mwa wale waliosemwa na marehemu Shaaban Robert  “Hawafi
wafao watu waliotenda mambo mema kwa jamii zao.”

Tunapoteza uelekeo kuhusu kuwatambua mashujaa wetu mfano ni katika
sekta ya usanii Marehemu Faraji Husein Katalambula  ana mchango
mkumbwa kutokana na kitabu chake cha riwaya ya simu ya kifo Kitabu
kilichotumiwa na mamilioni ya wanafunzi katika miaka ya 1970 kwenye
mitihani ya kidato cha nne

Lakini siku alipofariki viongozi wa kitaifa hawakumwona kuwa ni mtu
muhimu  kwa nchi yetu na hakuna hata taasisi moja ya serikali
iliyogharamia mazishi yake. Lakini tumeshuhudia muda mfupi baada ya
kifo cha Katalambula serikali ilijitosa kugharamia mazishi ya Stephen
Kanumba kwa  mamilioni ya fedha.

Wakati fulani kulikuwepo na mswada wa maziko ya kitaifa kwa viongozi
wakuu wa kitaifa Hatujui mchakato huo umekwamia wapi.Vivyo hivyo
kungekuwepo na mazishi ya mashujaa kwenye makaburi yatakayotengwa kila
mkoa ili iwe rahisi kwa taifa kuwa na utunzaji wa kumbukumbu za
mashujaa wetu popote walipo




Makumbusho ya taifa ni mahali pengine panapopaswa kuwa chimbuko la
kutunza kumbukumbu za mashujaa wetu tungetarajia mashuja wetu si wale
akina Mtemi Mkwawa, Mirambo, Mangi, Sina, Mareale na wengineo bali
kila kizazi kuna watu jasiri waliojitoa mhanga nao wanapaswa kuingizwa
kwenye rekodi hizo

Nchi ispokuwa  na utamaduni wa kuwaenzi na kuwathamini waliotoa
mchango mkubwa wakati wa enzi zao ni dhahiri kitarithisha maadili mema
ambayo yanayotoweka kila kukicha kwani tutasahau mashujaa
waliojulikana kwa uadilifu na mapenzi kwa nchi yao na badala yake
kuwaenzi wapenda rushwa kuwa mashujaa wetu

No comments:

Post a Comment