Friday, June 22, 2012

UBADHILIFU WA MALI ZA UMMA NI TATIZO KWA WANANCHI WA KIPATO CHA CHINI

kuwepo kwa mfumo dume wa ubadhilifu wa mali za umma ni tatizo linaloendelea kuumiza wananchi wenye kipato cha chini hali inayopelekea kukata tamaa ya kufikia malengo ya kuishi maisha bora.

Kufuati kuwepo kwa hali hiyo wananchi wamekuwa wakijiuliza maswali mengi na hasa wanapotaka rasirimali zilizopo katika taifa hili la Tanzania lakini hakuna majibu ya moja kwa moja ambayo wanapata.


Leo hii kwa mara nyingine tena watanzania wanashuhudia Bajeti ambayo bado haijaonyesha sura ya kumsaidia mtanzania hasa mwenye kipato cha chini ambaye anakula mlo mmoja kwa siku badala yake anaongezewa ugumu na ukali wa maisha .

Mtanzania huyu ambaye anategemea kula chispsi kavu huku akishushia soda ama maji ya kunywa ya shilingi mia mbili (300)leo hii gharama za ongezeko ya vinywaji hivyo ziko juu sasa tuatasema bajeti inamkomboa mwananchi wakipato cha chini ama vipi?

Hali hiyo imeendelea kuwaduwaza wananchi hawa lakini huku wakijiuliza maswali mengi kuwa kwanini gharama hizo zote zisielekezwe kwenye rasirimali zilizopo kama madini tunayomiliki ikiwemo Tanzanite,almasi, chuma, dhahabu, Uraniam na gesi ambazo zimeshindwa kuliongezea pato taifa na kutegemea misaada kwa wahisani.

Amakweli mbuzi wa maskini yake kamba tumekosa ubunifu na kutumia elimu ya mazoea katika kujikwamua na umaskini huu lakini hata kutumia fursa tulizonazo hasa katika kuzitumia vyema nyadhifa zetu na rasilimali zetu hasa misitu utalii na hifadhi za taifa.

Serikali imekua ikiendeleza miradi mbalimbali ya kijamii ambayo hutumia pato la taifa kwa lengo la kuhakiisha jamii inapata huduma bora nyingi kati ya miradi hiyo inapitia katika Halmashauri zetu za wilaya na mikoa huku ikichangiwa na wananchi na mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF.

Kupitia miradi hiyo na ripoti kadhaa za mapato na matumidhi ya fedha kwa mwaka uliopita na ujao huiladhimu kila halmashauri kuwasilisha ripoti ya bajeti ambayo ni mjumuisho wa bajeti kuu.

Nasema haya baada ya kuona mengi yaliyojili katika vikao vya kamati za Bunge ambavyo vimekuwa vikiendeshwa jijini Dar es salaam na kuhamia Dodoma baada ya Bunge la nane kuanza mwezi huu juu ya mjadala wa bajeti.

Naweza kuzipongeza kamati hizo kwa umakini wake uliopelekea kubaini mengi katika utendaji wa kazi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo zile hesabu na matumizi ya maendeleo ya bajeti zilizopita kwa Halmashauri zetu.

Ama kweli Watanzania kupitia kamati hizi tumebaini zimwi likujualo halikuli likakwisha tunalia na mafisadi wa Richmond na Epa kumbe kuna mafisadi hadi wa mayai ya kuku tunaofuga wenyewe.

Katika vikao hivyo kamati ya hesabu za Serikali za mitaa na halmashauri ikiwa ni idadi ya vikao vingi vilivyoendeshwa na makamu mwenyekiti wa kamati hiyo Bw.Idd Azzan iliibua uozo mwingi wa ubadhilifu wa fedha katika halmashauri mbalimbali ikiwemo ile ya Tunduru ambayo iliwaona wajumbe wa kamati hiyo ni watalii wasiojua hata bei ya yai la kuku na kuandika katika vitabu vya hesabu za halmashauri hiyo kuwa imetumia pesa za kodi za Watanzania wenye maisha duni kwa ajili ya chakula katika moja ya vikao vyao huku yai likiainishwa kununuliwa kwa shilingi 900 kila moja.

Tunatambua kuwa mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe na mtaji wa Watanzania walio wengi hasa wananchi wa vijijini katika halmashauri ya Bagamoyo ni kilimo huku afya ikiwa ni msingi imara wa utafutaji wa ridhiki ya wananchi hao na uchumi kwa ujumla.

Katika vikao vilivyoendelea vya kamati hiyo pia vilibaini ubadhilifu katika halmashauri ya Bagamoyo kwenye uwasilishaji wa ripoti ya hesabu za miradi ya kilimo (Dadp) na afya ule wa Basket fund ambapo katika miradi hiyo mradi wa afya ulikuwa unagharimu kiasi cha shilingi milioni 570 huku wa kilimo ukiwa una gharama ya shilingi milioni 467 na ilionyesha wazi ubabaishaji wa taarifa za matumizi ya miradi hiyo.

Lakini mbali na hesabu zote hewa bado halmashauri hiyo haikuridhika ama wenye matumbo manene hawakuenea katika mgao na badala yake imeonekana pia halmashauri hiyo ikituhumiwa na wizi wa dhahiri wa shilingi milioni 15 ambazo uongozi wa halmashauri uliziainisha fedha hizo katika ununuzi wa kiwanja cha kujenga shule ya msingi huku ikieleweka wazi kuwa kiwanja hicho kilitolewa bure na wananchi.

Katika kamati hiyo iliwataka kutumia wiki mbili viongozi wa Halmashauri ya Bagamoyo kuhakikisha wanawasilisha ripoti yenye mahesabu ya mapato na matumizi sahihi iliyopitia kwa mkaguzi wa hesabu za Serikali (CAG) huku pia wakitakiwa kurudisha fedha za wananchi zilizopotea hewani katika ununuzi wa kiwanja hewa cha shule.

Hali hiyo hiyo ilijitokeza pia katika Halmashauri mbalimbali hivyo kuiradhimu kamati hiyo kufikia hatua ya kuwapa adhabu viongozi wake aidha kwa kuwakata 15% za mishahara na kuwapa barua za onyo huku idadi kubwa ikiwa ni halmashauri hizo kupewa muda wa kuandaa upya vitabu vyao.

Ninachojiuliza mimi inawezekana Serikali haikuajiri wataalamu mbalimbali katika Halmashauri zetu?na kama wapo nini kazi ya mkurugenzi mweka hazna mwandisi na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali CAG ?

Wengi wa viongozi wa Halmashauri hizo walikuwa wakiamuliwa na kamati kupeleka vitabu vya mahesabu kwa mkaguzi mkuu kabla ya kuvirudisha tena katika kamati je awali hawakutambua kama hesabu za vitabu hivyo zinatakiwa kupita kwa mkaguzi ama wanarudi na hesabu mpya za matumizi ya fedha za walipa kodi katika utayarishaji wa vitabu hivyo na kuongeza matumizi ya ulipwaji wa posho.

Hayo hayo yalijitokeza pia katika Halmashauri ya Tarime na nyinginezo ambapo kwa Tarime wao walipewa mwezi mmoja kuhakikisha wanawasilisha mikataba na vielelezo vya miradi na skabadhi ya manunuzi ya miradi katika bajeti iliyopita sambamba na uwasilishaji wa ripoti ya bajeti ya mwaka 2012-2013 kwa mkaguzi mkuu.

Katika Halmashauri hiyo pia imejitokeza ubabaishaji wa utekelezaji wa miradi ya mfuko wa barabra wa (MAM) ruzuku za maendeleo sambamba na mikataba isiyoeleweka iliyopo katika mradi wa barabara wa Bukenye -Nkerege mpaka Nyamongo huku ununuzi wa mafuta hewa ukiwa ni chachu kubwa waliyonayo.

Mbali na mashaka tuliyaona katika Halmashauri zetu kuna jambo la kusikitisha katika bodi za mashirika ya umma kama si hoja walizopewa TBS na kamati ya kudumu ya hesabu za Serikali na mashirika ya umma (POAC )ni lini wangechukua hatua juu ya leseni hewa aliyonayo wakala wa ukaguzi wa magari aliyepewa kazi ya ukaguzi kwa miaka mitatu kuanzia 2009 .

Mbali na ukaguzi huo bodi ya TBS pia ndio yenye dhamana ya kukagua bidhaa zote zinazoingia nchini kabla ya kutumika sipati jibu bidhaa mbovu na zisizo na viwango zinapitia milango gani na vipi wamiliki wake wanaendelea kujizolea pato huku afya za Watanzania zikiendela kuwa hatarini.

Aidha kutokana na changamoto ya bajeti ndogo ya matumizi ya kawaida inayowaumiza Watanzania vipi bodi hiyo inawachukulia hatua kwa kuwatoza faini kubwa wamiliki wa viwanda vya bidhaa feki kama Omo,mbolea na mafuta ya magari na sabuni nyingine zilizoainishwa ili kuliongezea pato taifa.

katika mashirika ambayo yanawaumiza Watanzania walio wengi na kujiuliza mali nyingi zilizokuwa zikimilikiwa na shirika Usagishaji la Taifa NMC wapi zimepotelea ama kubinafsishwa likiwa liliundwa ili kuwa mkombozi wa Wananchi.

NMC ni taa ya kibatari iliyo na mwanga na kufifia ghafla na kunaibuka mjadala kuwa shirika hilo liko hai na linaendelea na kazi pasipo kuonekana mchango wake katika lengo lililokusudiwa.

Shirika hili tangu kuanzishwa kwake mwaka 2008 halikuwa na taarifa zozote kwa wananchi ukiachilia mbali taarifa ya mashine,kinu cha kusagishia na kiwanja namba 10 ambavyo vilinunuliwa na Serikali lakini hata umiliki wake wa nyumba ambazo zinapangishwa kwa wananchi bila hesabu kujulikana zilipo.

Cha kushauri Serikali kupitia upya bajeti hizo katika matumizi yake kabla ya kuandaa bajeti nyingine huku ikiwa makini katika utendaji wa viongozi wa juu wa taasisi na mashirika ya umma sambamba na ukaguzi yakinifu wa miradi na matumizi ya mapato ya ndani ya huduma za jamii.

Huduma za jamii ni mihimili muhimu katika bajeti ya nchi hivyo ubabaishaji wa ripoti za matumizi na uombaji wa hesabu mpya za Bajeti katika halmashauri itaigharimu Serikali kutokana na hesabu hewa zilizopo.

Aidha vyanzo vikuu vya mapato pia ni vyema kuwa chachu ya uchumi imara hivyo ipo haja ya kutumia rasilimali za nchi katika kuongeza pato la bajeti ili kufikia dhana ya maisha bora kwa kila Mtanzania

.




No comments:

Post a Comment