KLABU ya Simba, imetangaza rasmi kusitisha
mkataba wa kiungo wake, Salum Machaku kwa ajili ya maslahi ya klabu na
ya mchezaji mwenyewe.
Mbali na hilo, Kocha Mkuu wa timu hiyo,
Milovan Cirkovic anatarajia kutua nchini Ijumaa akitokea mapumzikoni
nyumbani kwao Serbia, huku wachezaji wa kigeni 'Maproo' nao wanatarajia
kuanza kuwasili siku hiyo.
Akizungumza na gazeti hili Makamo Makuu ya
klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa klabu
hiyo Ezekiel Kamwaga, alithibitisha kuachwa kwa Machaku kwa kusema
kiungo huyo sasa ni mchezaji huru.
"Ni kweli Simba imeamua
kusitisha mkataba na Machaku kwa maslahi ya klabu na yake binafsi, hivyo
kuanzia hivi sasa huyo ni mchezaji huru na timu yoyote inaweza
kumsajili," alisema Kamwaga.
Alipotakiwa kuanisha zaidi sababu za
kusitisha mkataba wa kiungo huyo, Kamwaga alisema ni uamuzi wa kawaida
ambao wamefanya kama walivyofanya kwa wachezaji wengine na ndiyo maana
wameangalia maslahi yake na ya klabu pia.
Mbali na hilo, Kamwaga
alisema Cirkovic pamoja na wachezaji Felix Sunzu na Emmanuel Okwi
wanatarajia kutua nchini kati ya Alhamisi na Ijumaa ambapo moja kwa moja
watajiunga na wenzao walioko kambini.
Akizungumzia suala la
kambi, Kamwaga alisema wana wiki ya pili tangu timu hiyo iingie kambini
ambapo walianza kwa kuingia 'gmy' na jana jioni walitarajia kuanza
mazoezi ya uwanjani kwenye viwanja vya Sigara, Dar es Salaam.
Alisema
katika mazoezi hayo ndipo watakapoonekana wachezaji wao wapya
waliowasajili msimu huu kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Kagame
ambalo linatarajiwa kuanza rasmi Julai 14, mwaka huu.
source: http://www.majira-hall.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment