SAA mbili
baada kukabidhiwa zawadi ya gari aina ya Corolla kwa kuibuka bingwa wa mkanda
wa Afrika wa IBF, ya bondia Francis Cheka alinusurika kifo kwenye ajali
ya gari aliyopata eneo Manzese jijini Dar es Salaam.
Cheka alikabidhiwa gari hiyo juzi saa tano usiku ikiwa ni zawadi ya mshindi baada ya kumchakaza Mada Maugo kwa TKO raundi ya saba na usiku huo wa saa saba gari hilo lilipata ajali kwa kumgogo mwendesha pikipiki maeneo ya Manzese.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kufafanua kuwa ilikuwa kati ya gari ndogo iliyokuwa ikiendeshwa na Cheka na pikipiki maarufu kama boda boda.
Kenyela alisema Cheka alikuwa akitokea mjini kuelekea Ubungo akiwa barabara kuu pikipiki hiyo iliyokuwa na mtu mmoja ilikatisha mbele ya gari hilo na kugongana.
"Dereva wa bodaboda aliumia na kukimbizwa hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu, lakini Cheka ni mzima hajaumia," alisema Kenyela na kusisitiza kuwa uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea.
Rais wa Organizesheni ya Masumbwi ya TPBO, Yassin Abdallah alisema gari hiyo ni ile iliyotolewa kwa ajili ya zawadi kwa mshindi wa pambano lake na Maugo.
Abdallah alisema kwa taarifa alizonazo ni kwamba Cheka alikuwa akimsindikiza mmoja wa watu wake Manzese baada ya kumalizika kwa pambano
Hata hivyo, habari zisizo rasmi zilieleza kuwa baada ya ajali hiyo Cheka alikutana na kizazaa cha kusota rumande usiku huo kabla ya kuruhusiwa jana asubuhi.
No comments:
Post a Comment