KAMPUNI ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imetangaza kujivunia wingi wa ajira ambazo imetengeneza kwa watanzania tangu kuanzishwa kwake. Kampuni hiyo imeajiri asilimia kubwa ya watanzania katika ajira za moja kwa moja na zile zisizo za moja kwa moja. Dar es Salaam 14 Agosti 2012
Taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Bw. Rene Meza , alitaja maeneo mbalimbali ambayo kampuni hiyo imetoa ajira kwa wingi na kutanabaisha kuwa huduma ya m – pesa imetengeneza ajira zaidi ya elfu ishirini na tano kwa watu wa makundi mbalimbali.
“Kama kampuni tuna ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, kupitia huduma yetu ya m-pesa sasa tumetengeneza ajira zaidi ya elfu ishirini na tano hapa nchini mijini na vijijini. Hii ni hatua kubwa sana katika sekta ya ajira. Kwa kuwa huduma hii imeshika hatamu katika huduma za kifedha bado watu wengi zaidi wanaendelea kujiunga na uwakala. Kwa mwezi sasa tunapata maombi ya uwakala zaidi ya 2000 hivyo tunatarajia ajira hizi kuongezeka kwa kasi,”alisema
Bw. Meza alibainisha sehemu nyingine ambazo kampuni hiyo imetoa ajira kwa Watanzania zaidi kwa kusema sasa kumekuwa na wafanyabiashara wa kujitegemea wapatao elfu sita ambao wamejiajiri kwa kuuza muda wa maongezi na kadi za simu.
“Tumegundua kuwa Watanzania wengi wanaweza kujiajiri na kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo. Tunaona kwa kiasi kikubwa watu waliojiajiri kuwa mawakala wanaendelea vizuri, hivyo tumetengeneza mfumo ambao utaendelea kutoa ajira zaidi za kujitegemea kwa Watanzania na mpango wa kutoa elimu ya biashara kwa watu hawa,” alieleza Bw. Meza
Amesema kuwa kampuni hiyo sasa imetoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya 450 na kutoa kipaumbele kwa wanawake ambao wanaongoza vitengo mbalimbali vya kampuni hiyo.
“Tunajitahidi kutoa kipaumbele sana kwa wanawake na tumeona kweli wana uwezo mkubwa katika utendaji wao. Kampuni sasa inaendelea kukua kwa kasi na sisi tutaendelea kuthamini mchango wa kila mmoja katika kuchangia maendeleo na ukuaji wa kampuni ya Vodacom Tanzania,”
No comments:
Post a Comment