Wednesday, August 15, 2012

TBS KUKAGUA BIDHAA

SHIRIKA la Viwango Nchini (TBS) limesema kuwa litahakikisha ukaguzi wa nje wa bidhaa unaimarika ili kuepukana na kuingizwa kwa bidhaa feki na kusababisha gharama zisizokuwa na msingi.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam juzi na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi Bw. Razaro Msasagala wakati wa kuteketeza kwa moto bidhaa zilizoingizwa nchini zikiwa chini ya kiwango.


Bidhaa hizo ni pamoja na pampasi za watoto na pad za wanawake zenye thamani ya Tsh. milioni 18 ambazo ziliingizwa nchini kutoka China Desemba mwaka jana.

Bw. Msasagala alisema kuwa TBS imegharamia Tsh. milioni 4 ikiwa ni pamoja na gharama za utoaji wa bidhaa hizo na uteketezaji baada ya mmiliki wake kukimbia kutokana na kukwepa kodi ya kuifadhi ya dola za Marekani milioni 18.

"Ukaguzi wa nje ukiimarishwa utasaidia kuepukana na gharama zisizokuwa na msingi kama ambavyo tumetumia Tsh. milioni 4 kwa ajili ya kuteketeza bidhaa hizi ili kuhakikisha kuwa haziingii mtaani jambo ambalo linaweza kusababisha madhara ya kiafya wa watumiaji," alisema Bw. Msasagala

Alisema kuwa bidhaa hizo ziliingia bandarini kabla ya mfumo mpya wa ukaguzi haujaanza kutumika ambapo mfumo huo ulianza kutumika Februari mwaka huu.

Hata hivyo Bw. Msasagala alisisitiza kuwa ukaguzi wa nje ukiimarika pamoja na kuwepo wa mfumo mpya wa ukaguzi itasaidia uingizwaji wa bidhaa zisizokuwa na ubora jamboa ambalo linasababisha hasara na madhara kwa watumiaji.

No comments:

Post a Comment