Julai 13,
2012 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliwasilisha Maoni yake kuhusu Mpango na
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha
2012/2013. Pamoja na mambo mengine, Maoni ya Kambi yalihusu utaratibu wa uteuzi
wa majaji wa Mahakama ya Tanzania.
Maoni ya
Kambi yalizua mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge huku wachangiaji wengi
wakimtuhumu Msemaji wa Kambi kwa “kuidhalilisha” Mahakama na/au “kuwadhalilisha
majaji” (Gosbert Blandes-Karagwe CCM); “kuwavunjia heshima majaji” (Naibu Spika
Job Ndugai); kuwatukana na kuwadhalilisha majaji (Murtaza Mangungu-Kilwa
Kaskazini); “kuwa-offend, kuwadhalilisha na kuwanyanyasa majaji” (Assumpter
Mshama-Nkenge CCM); “kufedhehesha Mahakama na majaji” (Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Frederick Werema).
Aidha,
Msemaji wa Kambi alishambuliwa kwa kudaiwa kuwa mfitini na asiye na akili
timamu (Muhammad Chomboh- Magomeni CCM)); na “kujiamini kwamba yeye anajua
zaidi kuliko watu wengine wote” (Mangungu). Kwa upande wake, Waziri wa Katiba
na Sheria, Mathias Chikawe alilihakikishia Bunge kwamba “... haijatokea hata
siku moja katika nchi hii Rais akamteua Jaji wa Mahakama Kuu bila kuzingatia
mapendekezo yaliyopelekwa kwake na hii Tume ya Uajiri wa Mahakama.” Zaidi ya
hayo, “... labda Mheshimiwa Lissu anamjua Jaji angalau mmoja na anaweza
akamtaja aseme Jaji huyu ametolewa tu mitaani na Mheshimiwa Rais, yupi hakuna…
hawa majaji wote walioteuliwa wamepitia mchakato huu wa kikao kizito sana cha
watu ambao ndiyo wenye sheria ya nchi hii.”
Baadaye
Msemaji wa Kambi alitakiwa kufuta kauli yake kuhusu uteuzi wa majaji usiofuata
utaratibu uliowekwa na Katiba. Msemaji wa Kambi alikataa kufuta kauli hiyo
ambako Mwenyekiti wa Kikao alielekeza Msemaji wa Kambi apelekwe kwenye Kamati
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa hatua zaidi. Alichukua uamuzi huo ili
masuala hayo yapatiwe ufafanuzi ili wananchi wapate picha kamili na ya kweli
kuhusu jambo hili muhimu. Maelezo haya yana lengo la kutoa ufafanuzi huo.
Katika
maelezo yake kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya BUnge, Lissu alisema,
“Nitajitahidi kwa kadri inavyowezekana kutoa ushahidi unaothibitisha kwamba
siyo tu kwamba utaratibu wa kikatiba katika uteuzi wa majaji umekiukwa mara
nyingi, bali pia majaji wengi walioteuliwa kwa utaratibu wa nje ya Katiba
wamekuwa hawana ‘uwezo, ujuzi na kwa kila hali hawakufaa kukabidhiwa Madaraka
ya Jaji wa Mahakama Kuu.”
TATIZO LA
MUDA MREFU
Kuna
ushahidi mkubwa kuthibitisha kwamba kuna watu wameteuliwa kuwa Majaji wa
Mahakama Kuu “... wakiwa wamekaribia muda wao wa kustaafu kwingineko katika
utumishi wa umma (na) wanapewa ‘zawadi’ ya ujaji ili kuwawezesha kupata mafao
ya majaji wastaafu ambayo yameboreshwa sana katika miaka ya karibuni.” Ni
muhimu kuweka wazi hapa kwamba utamaduni huu haukuanza baada ya Rais Jakaya
Kikwete kuchaguliwa kuwa Rais, bali ni tatizo la muda mrefu. Kwa mfano,
marehemu Jaji Kulwa Masaba na Jaji Madina Muro na majaji Stephen Ihema, Juxton
Mlay, Augustine Shayo na Vincent Lyimo waliteuliwa majaji wa Mahakama Kuu baada
ya utumishi wa muda mrefu kwingineko katika utumishi wa umma.
Majaji
Masaba na Muro waliteuliwa huku wakiwa wagonjwa mahututi na – kwa kadri
ninavyofahamu - hawakuwahi kuandika hukumu hata moja kabla ya mauti kuwafika!
Jaji Lyimo aliteuliwa Machi 28, 2007 mwaka mmoja kabla ya muda wake wa kustaafu
kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, ilipofika Oktoba 26, 2007 Katibu Mkuu
Kiongozi wakati huo Phillemon Luhanjo alimtaarifu Jaji Mkuu kwamba Rais Kikwete
“... ameamua kusogeza mbele muda wa kustaafu wa Mheshimiwa Jaji Vincent Kitubio
Damian Lyimo kwa miaka mitatu kuanzia Machi 28, 2008 siku ambayo angestaafu kwa
lazima”!
Kwa
upande wao, Majaji Ihema, Mlay na Shayo walijizolea umaarufu kwa kuwa majaji
wasioandika hukumu na hivyo kuwa wacheleweshaji wakubwa wa kesi katika Mahakama
Kuu. Jaji Ihema alitia fora kwenye jambo hili kiasi kwamba Juni 16, 2003
Mwenyekiti wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Mzee Joram
Allute, alilazimika kumwandikia Rais Benjamin Mkapa maombi ya kumwondoa Jaji
Ihema kama Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania “kwa uzembe na kukosa maadili.”
Mzee
Allute alikuwa na kesi kwa Jaji Ihema ambapo Jaji huyo ‘alikalia’ uamuzi kwa
zaidi ya miaka minne hadi aliponyang’anywa faili la kesi hiyo na kukabidhiwa
Jaji mwingine aliyeandika uamuzi ndani ya wiki tatu! Mwezi mmoja kabla ya barua
ya Mzee Allute kwa Rais Mkapa, mawakili wake walikuwa wamemwandikia Jaji Mkuu
Barnabas Samatta kulalamikia ucheleweshaji wa uamuzi wa kesi hiyo. Mawakili hao
walidai: “Hadhi na heshima ya Mahakama inaporomoka vibaya kama inachukua zaidi
ya miaka mitatu kwa Jaji kutafakari na kutoa uamuzi kwa jambo jepesi kama
maombi ya pingamizi.” Licha ya malalamiko haya dhidi yake, Jaji Ihema alipatiwa
mkataba wa ajira wa miaka miwili mara baada ya kustaafu mwaka 2005.
MAJAJI WA
MIKATABA
Agosti 2,
2005 Jaji Kiongozi Hamisi Msumi alitoa taarifa kwa majaji wote wa Mahakama Kuu
kwamba Jaji Ihema alikuwa amepewa mkataba mpya baada ya kustaafu kama Jaji wa
Mahakama Kuu. Taarifa hiyo ilimfanya Jaji Bernard Luanda, wakati huo Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, kuhoji ‘Uhalali Kikatiba kwa Majaji Kufanya
Kazi kwa Mkataba Baada ya Kustaafu.’ Katika taarifa yake kwa Jaji Kiongozi
Msumi, Jaji Luanda alisema kwamba “... suala la majaji kupewa mikataba ...
linaenda kinyume na Katiba.” Jaji Luanda alifafanua: “Kwa kuwa Jaji amestaafu,
basi kiapo chake nacho kimeondoka. Kwa bahati mbaya hawaapishwi ili washike
kazi hizo za ujaji.... Ni hoja yangu kwamba Majaji waliostaafu na kupewa
mikataba si Majaji kwa mujibu wa Katiba.”
Msimamo
wa Jaji Luanda uliungwa mkono mwaka mmoja baadaye na Jaji wa Rufaa, Augustino
Ramadhani wakati huo akiwa Kaimu Jaji Mkuu. Katika ‘Mawazo Kuhusu Vifungu
Vinavyohusu Mahakama na Majaji’ aliyomwandikia Jaji Mkuu Samatta na kunakiliwa
kwa Majaji wa Rufaa wote, Jaji Ramadhani alisema kwamba “... sio sahihi kwa
Jaji Mkuu kustaafu na kupewa mkataba wa kuendelea na wadhifa huo kupindukia
umri wa miaka 65 (ambao ndio umri wa kustaafu kwa lazima kwa Jaji wa Rufaa na
Jaji Mkuu).” Baadaye Jaji Luanda aliteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa wakati Jaji
Ramadhani alikuja kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
Kauli ya
Kambi kwamba kuna ukiukaji mkubwa wa Katiba kuhusiana na uteuzi wa majaji
inaungwa mkono na nyaraka za ndani ya Serikali na hasa Ofisi ya Rais, Ikulu
yenyewe. Desemba 6, 2007, mkutano kuhusu ajira ya majaji waliostaafu ulifanyika
Ikulu, Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu Kiongozi Luhanjo.
Wajumbe wengine walikuwa pamoja na Mwanasheria Mkuu Johnson Mwanyika na Naibu
wake Sazi Salula, Katibu Mkuu Utumishi George Yambesi, Msajili wa Mahakama ya
Rufani, Sophia Wambura na Susan Mlawi wa Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri.
Kwa
mujibu wa Kumbukumbu za Mkutano huo, “kwa utaratibu unaotumika sasa, baadhi ya
Majaji wanaofikisha umri wa kustaafu kwa mujibu wa Ibara ya 110(1) kwa Majaji
wa Mahakama Kuu na Ibara ya 120(1) ya Katiba wanaongezewa muda wa kuendelea na
utumishi wao kwa mkataba baada ya wao kuwasilisha maombi rasmi.” Baada ya
mjadala juu ya jambo hili, wajumbe wa mkutano walikubaliana kwamba “utaratibu
wa kuongeza muda kwa njia ya mkataba unakiuka masharti ya Katiba na kuleta
mkanganyiko kama Majaji hao wanastahili kulipwa mshahara au pensheni au vyote
kwa pamoja.”
Matokeo
ya mkutano wa Ikulu ilikuwa ni kuundwa kwa ‘Kikundi Kazi kwa Ajili ya Kuchambua
na Kushauri Kuhusu Ajira ya Majaji Baada ya Kustaafu’ chini ya Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Kikundi Kazi kiliwasilisha Taarifa yake Machi
7, 2008. Katika Taarifa yake Kikundi Kazi kinakubaliana na msimamo amo wa kikatiba
kwamba “kwa kuzingatia Ibara za 110 na 120 za Katiba inaonekana wazi kuwa suala
la ajira za mikataba kwa Majaji ambao wamekuwa wakifanya kazi za Jaji baada ya
kufikia umri wa kustaafu ni kinyume cha Katiba.” Kwa mujibu wa Taarifa hiyo,
hadi mwezi Machi 2008, “... walikuwepo Majaji wawili ... wa Mahakama ya Rufani
na Majaji tisa ... wa Mahakama Kuu, ambao wapo katika ajira za mkataba, na Jaji
mmoja ... wa Mahakama Kuu aliyeongezewa muda wa ajira kwa mujibu wa masharti ya
Katiba....”
Hii ina
maana kwamba, kulikuwa na Majaji kumi na moja ambao walikuwa wanafanya kazi
kinyume cha Katiba na – kwa maneno ya Jaji wa Rufaa Luanda – hawakuwa Majaji
kwa mujibu wa Katiba! Aidha, kwa mujibu wa ushahidi wa nyaraka hizi, kulikuwa
na Jaji mmoja tu ambaye alikuwa ameongezewa muda wa ajira ya ujaji kwa mujibu
wa Katiba. Katika mapendekezo yake, Kikundi Kazi hakikumung’unya maneno:
“Mikataba
iliyopo hivi sasa iko kinyume cha Katiba.... Hii ina maana kwamba Majaji hao
wanafanya kazi ya Jaji kinyume cha Katiba, hivyo kazi zote ambazo wamezifanya
na wanaendelea kuzifanya wakiwa chini ya ajira mpya za mikataba hazina uhalali
wowote kisheria. Kazi hizo ni sawa kama vile zimefanywa na mtumishi mwingine
yeyote asiye na madaraka ya Jaji. Hivyo basi, Rais ashauriwe kuifuta mikataba
hiyo mara moja kwa vile ina madhara makubwa kwa jamii na katika uteuzi wa
Majaji wapya kuchukua nafasi zao. Majaji waliofutiwa mikataba waendelee na
pensheni zao kama kawaida.”
Miaka
minne imepita tangu Kikundi Kazi kiwasilishe mapendekezo yake Ikulu lakini
hakuna hatua zilizochukuliwa kutekeleza mapendekezo hayo. Aidha, licha ya
msimamo wa majaji Luanda na Ramadhani kuwa na umri wa takriban miaka saba,
utaratibu wa uteuzi wa majaji wastaafu haujaachwa na mamlaka husika ya uteuzi.
Ajira ya sasa ya Jaji Kiongozi Fakih Jundu iko katika kundi hili la watu
wasiokuwa Majaji kwa mujibu wa Katiba.
JAJI
KIONGOZI FAKIH JUNDU
Jaji
Kiongozi Fakih Jundu aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Rais Mkapa mwaka
2003. Julai 29, 2009, Jaji Jundu wakati huo akiwa Jaji Mfawidhi wa Kanda ya
Iringa, alitoa taarifa ya kustaafu kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, mara baada
ya kutoa taarifa hiyo, Jaji Jundu siyo tu alipewa mkataba wa ujaji kwa miaka mitatu,
bali pia alipandishwa cheo na kufanywa Jaji Kiongozi.
Kama hiyo
haitoshi, inasemekana sasa kwamba Jaji Kiongozi Jundu ameongezewa mkataba
mwingine tena wa miaka miwili kuendelea kuwa Jaji Kiongozi kuanzia Julai 29,
2012! Huu ni ukiukaji wa Katiba. Kwanza, kwa mujibu wa Taarifa ya Kikundi Kazi,
“... umri wa kustaafu wa Jaji Kiongozi ni miaka sitini.... Hivyo, iwapo Rais
atamuongezea Jaji Kiongozi muda wa kufanya kazi, hatamuongezea kama Jaji
Kiongozi.”
Kwa maana
nyingine, kama ilikuwa makosa kikatiba kumpa Jaji Jundu mkataba wa ajira kama
Jaji wa kawaida, ilikuwa makosa makubwa zaidi kikatiba kumpandisha cheo na
kumfanya Jaji Kiongozi wakati alikwishafikisha umri wa kustaafu wa Jaji
Kiongozi! Pili, kwa utamaduni uliozoeleka Tanzania, majaji wamekuwa wanaongezewa
kipindi kimoja cha miaka miwili ili wamalizie kesi walizokuwa nazo hadi muda
wao wa kustaafu unawadia. Kwa msimamo wa kikatiba ulioelezwa na Jaji wa Rufaa
Luanda, Jaji Mkuu Ramadhani na Kikundi Kazi, siyo sahihi kwa Jaji Kiongozi
Jundu kustaafu na kupewa mkataba wa kuendelea na wadhifa huo kupindukia muda
wake wa kustaafu kwa mujibu wa Katiba!
Nyongeza
hii ya pili ya mkataba wa Jaji Kiongozi Jundu imewafanya watu wanaojiita
‘Watumishi wa Mhimili wa Mahakama’ kumwandikia Msajili wa Mahakama ya Rufani ya
Tanzania kulalamikia jambo hilo. Kwa mujibu wa barua yao, ambayo pia
ilinakiliwa kwa Mwanasheria Mkuu na Jaji Mkuu, watu hao wamesema yafuatayo
kuhusu Jaji Kiongozi Jundu: “Sisi watumishi wa Mahakama tunafahamu udhaifu
mkubwa kiutendaji alionao Jaji Kiongozi wetu wa sasa. Kimsingi hamudu madaraka
haya. Ipo mifano mingi ya udhaifu wa Jaji Jundu. Mfano alimhamisha hakimu
kutoka kituo chake cha kazi kama adhabu kwa vile hakimu huyo alitoa maamuzi
ambayo yeye hakuyafurahiya kwenye ile kesi maarufu ya kibaragashia. Ni busara
za Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, ndizo zilizomsaidia hakimu huyo.”
JAJI
THOMAS MIHAYO
Thomas
Bashite Mihayo aliteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Oktoba 8, 2003.
Januari 16, 2006 Jaji Mihayo alitoa notisi ya kustaafu kwa mujibu wa Katiba
kuanzia Juni 8, 2006 atakapokuwa ametimiza umri wa miaka sitini. Hata hivyo,
Machi 8 ya mwaka huo, Jaji Mihayo alitaarifiwa na Jaji Mkuu kwamba Rais Kikwete
alikuwa amempa “... mkataba wa miaka miwili kuanzia Juni 9, 2006.” Mkataba huo
ulifikia mwisho wake Juni 8, 2008. Hata hivyo, Jaji Mihayo alipatiwa mkataba
mwingine tena wa mwaka mmoja ulioanzia Juni 9, 2008 hadi Juni 8, 2009 na baada
ya hapo hakupatiwa mkataba mwingine.
Inaelekea
Jaji Mkuu Ramadhani alisahau msimamo wake wa awali kuhusu ajira za mikataba
kwani ndiye aliyependekeza Jaji Mihayo “... apewe mkataba mwingine wa mwaka
mmoja...” Na wala si Jaji Mihayo pekee aliyepatiwa au kuongozewa mkataba katika
mazingira tatanishi kama haya. Kwa mujibu wa nyaraka za Idara Kuu ya Utumishi, Jaji
Donasian Mwita alipatiwa mkataba wa ujaji Juni 28, 2004. Mkataba huo wa miaka
miwili ulianza kutumika Julai 1, 2004. Vile vile, Jaji Joseph Masanche alisaini
mkataba wa aina hiyo hiyo na Idara Kuu ya Utumishi ulioanza kutumika kuanzia
Machi 7, 2006.
MAADILI
YENYE SHAKA
Msemaji
wa Kambi hakuzungumzia masuala yanayohusu maadili ya majaji. Hata hivyo,
kutokana na mjadala uliojitokeza ndani na nje ya Bunge kutokana na hotuba yake,
ushahidi umepatikana unaoonyesha kwamba baadhi ya majaji wameteuliwa bila ya
kwanza kuwafanyia uchunguzi juu ya maadili yao.
MAJAJI
KASSIM NYANGARIKA NA ZAINAB G. MURUKE
Kassim
Nyangarika alikuwa wakili wa kujitegemea na wakili mwenza wa Jaji Kiongozi
Jundu kabla ya uteuzi wake kuwa Jaji wa Mahakama Kuu mwaka 2003. Kama wakili,
Bwana Nyangarika aliwahi kumwakilisha mlalamikaji katika kesi ya Peter Muti
dhidi ya CIELMAC Ltd., Kesi ya Madai Na. 314 ya 2003 iliyofunguliwa katika
Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni. Katika kesi hiyo mteja wa wakili Nyangarika
alishinda.
Hata
hivyo, kufuatia rufaa dhidi ya uamuzi huo, Mahakama Kuu ilifutilia mbali
mwenendo wa kesi hiyo baada ya kugundua kwamba Wakili Nyangarika alikuwa
amefanya vitendo vyenye kuashiria uvunjifu mkubwa wa maadili. Kwa mfano,
Mahakama Kuu iligundua kuwa Wakili Nyangarika alimwelekeza hakimu – kwa kutumia
‘kipande cha karatasi cha rafu na kilichoandikwa kirafiki’ - namna ya kuendesha
kesi hiyo. Mahakama Kuu iligundua makosa makubwa zaidi ya hilo. Kwa mujibu wa
Jaji Kalegeya, “... kulikuwa na mawasiliano yasiyokuwa rasmi kati ya Mahakama
na Wakili.” Jaji Kalegeya alikuta ushahidi wa uwezekano mkubwa kwamba Wakili
Nyangarika ndiye aliyeandaa uamuzi wa Mahakama katika kesi hiyo. Aidha,
Mahakama Kuu iligundua kwamba Wakili Nyangarika “... aliielekeza Mahakama
kutokutoa uamuzi kwa tarehe iliyopangwa badala yake aliielekeza itoe uamuzi huo
tarehe nyingine.”
Kwa
mujibu wa Jaji Kalegeya, kama kilichoonyeshwa katika mawasiliano ya Wakili
Nyangarika na Mahakama ya Wilaya kilikuwa cha kweli basi “... utoaji haki
katika Mahakama hiyo uko katika hatari kubwa kama sio jina la Mahakama yote,
kitu kinachohitaji marekebisho ya haraka.” Kwa sababu hiyo, Jaji Kalegeya
alielekeza kwamba “mamlaka husika zichukue hatua za kufichua ukweli kuhusu
barua ya Wakili Nyangarika ya tarehe 18/03/2004.” Hukumu na maelekezo ya Jaji
Kalegeya yalitolewa tarehe 22 Julai, 2005. Miezi saba baadaye, Wakili
Nyangarika aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania!
Wakili
mwingine mwenye maadili ya mashaka yanayofanana na ya Jaji Nyangarika ambaye
pia ameteuliwa Jaji Mahakama Kuu ni Zainab Muruke. Kama wakili, Zainab Muruke
alimwakilisha Stephen Hill Forwood ambaye alikuwa amepatikana na hatia na
kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka miwili bila faini katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi ya Kisutu. Baadaye kampuni ya mawakili ya Z.G. Muruke & Co.
Advocates iliwasilisha Hati ya Mapitio (Memorandum of Review) katika Mahakama
hiyo hiyo ikiomba Bwana Forwood abadilishiwe hukumu.
Ombi hilo
lilikubaliwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Kabuta na tarehe 26 Julai, 2004, Bwana
Forwood akabadilishiwa adhabu kuwa faini ya shilingi 20,000 au kifungo cha
miaka miwili. Jambo hili liliripotiwa kwa Jaji Kiongozi ambaye aliamuru
uchunguzi ufanywe uliopelekea kushushwa cheo cha Hakimu Mkazi Kabuta. Jaji
Kiongozi pia aliamuru Wakili Muruke atoe maelekezo ya ushiriki wake katika
sakata hilo. Hiyo ilikuwa tarehe 14 Desemba, 2004. Mwaka mmoja na miezi miwili
baadaye, Zainab Muruke aliteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
MAJAJI
PELAGIA B. KHADAY NA PATRICIA FIKIRINI
Bi.
Pelagia B. Khaday ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliyeteuliwa mwaka 2009.
Kabla ya uteuzi huo Bi. Khaday alikuwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu na kabla ya hapo alikuwa Hakimu Mkazi Mkuu na Msajili wa Wilaya,
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha. Agosti 12, 2004, alipewa taarifa ya kusimamishwa
kazi kama Msajili wa Wilaya na kuhamishiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
kutokana na ‘uzito wa shutuma’ zilizotolewa dhidi yake kwa Jaji Mkuu.
Taarifa
hiyo iliandikwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Edward
Rutakangwa, kwa maelekezo ya Jaji Mkuu na ilieleza kwamba Bi. Khaday alikuwa
anatuhumiwa kwa “kuwashinikiza au kuwashawishi baadhi ya mahakimu mkoani Arusha
kushughulikia au kuamua kwa upendeleo mashauri yaliyowahusu ... jamaa au rafiki
zake”; na “kuwaandalia sababu za rufaa baadhi ya washitakiwa waliotiwa hatiani
na mahakama za mahakimu hapa mkoani.”
Kabla ya
kumsimamisha Bi. Khaday kazi, Jaji Mfawidhi Rutakangwa alikuwa amemteua
Mheshimiwa Jacob Somi, wakati huo akiwa Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha
Ardhi, kuwa Afisa Uchunguzi (Enquiry Officer) ili kuchunguza tuhuma dhidi ya
Bi. Khaday. Taarifa ya Uchunguzi wa Awali ya Afisa Uchunguzi Somi inasema
kwamba Bi. Khaday alikuwa amelalamikiwa na mahakimu kwa kuwashinikiza ili watoe
maamuzi ya kesi zilizokuwa zinawakabili jamaa au marafiki zake.
Kwa
mujibu wa Taarifa hiyo, Hakimu Mkazi Elvin Mugeta “alikiri kuwa-approached na
Bi. Khaday ili atoe hukumu ya upendeleo kwa mshtakiwa Richard Bareto ambaye
inasadikiwa kuwa ni jamaa wa rafiki yake wa karibu.” Ijapokuwa Bi. Khaday
alikanusha kufanya hivyo, Afisa wa Uchunguzi Somi aliridhika kwamba “Bi. Khaday
alikuwa amejiwekea utaratibu, kama alivyodai mwenyewe, wa kuwasiliana na
Mahakimu kwa lengo la kuwafahamisha pamoja na mambo mengine malalamiko yaliyokuwa
yakimfikia dhidi yao ili kuwanusuru wasiharibikiwe.”
Hata
hivyo, Afisa Uchunguzi Somi aliridhika kwamba “utaratibu huu ulikuwa kero kwa
mahakimu pale alipoutumia kwa kushinikizwa na jamaa zake na/au rafiki zake kwa
lengo la kupata maamuzi ya upendeleo. Kitendo cha kumtoa mahakamani Hakimu kwa
lengo la kutaka kujua hatima ya mshtakiwa Bareto aliyekuwa asomewe hukumu siku
hiyo, ni mfano wa matumizi mabaya ya utaratibu huo.”
Afisa
Uchunguzi Somi hakupata uthibitisho wa madai ya Bi. Khaday kuwaandalia sababu
za rufaa washtakiwa waliotiwa hatiani. Hata hivyo, kwa mujibu wa Taarifa yake,
“... sikuridhishwa na utaratibu wake wa kupeleka nakala ya hukumu kwa Bi. Mushi
na kumtaka aisome ili kuona kama kuna uwezekano wa mshtakiwa Hussein Ramadhani
Kitema kukata rufaa Mahakama Kuu baada ya kufungwa jela na Bw. Mugeta.” Afisa
Uchunguzi Somi alipendekeza kwamba Bi. Khaday – “ambaye ni mtumishi wa Mahakama
kwa kipindi kisichopungua miaka 20...” - apewe nafasi ya kujirekebisha.
Baada ya
kuwasilishwa kwa Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi, Jaji Mfawidhi Rutakangwa
alimteua Mh. Samuel Karua, Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, kuwa
Investigation Officer. Tarehe 23 Februari 2007, Investigation Officer Karua
aliwasilisha Taarifa ya Uchunguzi wake kwa Jaji Mkuu. Taarifa ya Investigation
Officer Karua ilimkosha Bi. Khaday kwa tuhuma zote dhidi yake.
Hata
hivyo, Taarifa ya Investigation Officer Karua ina maeneo mengi yanayoleta
mashaka. Kwanza, kama Investigation Officer Karua mwenyewe alivyosema, shahidi
muhimu katika uchunguzi wake alikuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Mushi. Vile vile,
shahidi huyu alikuwa ‘star witness’ katika uchunguzi wa awali mbele ya Afisa
Uchunguzi Somi na ndiye aliyetoa ushahidi wa yeye na mahakimu wengine
kuingiliwa katika kazi zao na Bi. Khaday.
Hata hivyo,
mbele ya Investigation Officer Karua, shahidi huyu muhimu alikana kila kitu
alichokisema mbele ya Afisa Uchunguzi Somi. Kwa kiasi kikubwa, Investigation
Officer Karua aliitumia about turn hii kumkosha Bi. Khaday dhidi ya tuhuma zote
zilizokuwa zinamkabili. Cha kushangaza ni kwamba Investigation Officer Karua
hakujiuliza na hakumuuliza shahidi huyu sababu za kukana ushahidi wote alioutoa
mbele ya Afisa Uchunguzi Somi.
Je,
alirubuniwa au kutishwa ili amsaidie Hakimu na mtumishi mwenzake katika
Mahakama ya Tanzania asifukuzwe kazi? Kama sio hivyo, je, ni sababu zipi
zilizomfanya shahidi huyu muhimu kubadili ushahidi wake kwa kiasi hicho? Je,
ushahidi alioutoa shahidi huyu mbele ya Afisa Uchunguzi Somi ulikuwa wa uongo?
Na kama ulikuwa wa uongo, ushahidi wake wa pili kwa Investigation Officer Karua
ni wa kweli kiasi gani mpaka kumfanya Investigation Officer Karua kutamka kuwa
shahidi huyu ‘anaweza ... kuwa anasema ukweli.’
Inaelekea
Investigation Officer Karua, Hakimu Mkuu Mkazi mwenye uzoefu wa miaka mingi
katika Mahakama, alifanya kazi yake kwa mtazamo wa kimahakama zaidi badala ya
kutumia mtazamo wa kiupelelezi na/au kiuchunguzi ambayo hasa ndiyo ilikuwa kazi
yake katika uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Bi. Khaday. Kwa mtazamo wa kimahakama,
ukweli kwamba shahidi muhimu kama Hakimu Mkazi Mfawidhi Mushi alikana ushahidi
wake wa awali mbele ya Afisa Uchunguzi Somi ilikuwa inatosha kumfutia Bi.
Khaday hatia yote. Kwa mtazamo wa kiupelelezi/kiuchunguzi, about turn ya
shahidi huyu ingemfanya Investigation Officer Karua kuchunguza zaidi sababu za
kigeugeu hicho.
Pili,
Investigation Officer Karua hakuipa uzito wa kutosha Taarifa ya Afisa Uchunguzi
Somi. Kwa mfano, Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi – yenye kurasa 14 zilizochapwa
- imeelezewa katika Taarifa ya Investigation Officer Karua kwa aya moja tu! Kwa
sababu hiyo, ni vigumu kukubaliana na Investigation Officer Karua kwamba
Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi ‘ilikuwa muhimu sana’ wakati umuhimu huo
haujafafanuliwa wala kuelezewa hata kidogo katika Taarifa yake.
Aidha,
Investigation Officer Karua alitakiwa kueleza sababu za kutofautiana na Afisa
Uchunguzi Somi kwamba Bi. Khaday alikuwa anakera mahakimu kwa kuwasiliana nao
baada ya kushinikizwa na ndugu au rafiki zake ili wapatiwe upendeleo katika
kesi zilizokuwa zinawakabili. Investigation Officer Karua hakufanya hivyo. Vile
vile, Investigation Officer Karua hakuona ajabu wala kujiuliza kama ilikuwa ni
kitu cha kawaida kwa Bi. Khaday kumleta Richard Bareto – mshtakiwa
aliyehusishwa na shinikizo la Bi. Khaday kwa Hakimu Mkazi Mugeta – kama shahidi
wake wa utetezi.
Tatu,
Investigation Officer Karua hakutoa sababu za maana za kutochukua ushahidi wa
mahakimu wengine waliodaiwa kushinikizwa na Bi. Khaday. Katika aya moja tu
iliyowahusu mahakimu hao, Investigation Officer Karua alisema kwamba siku ya
kutoa ushahidi wao kwake, watu hao “... walishikilia msimamo wa kauli walizotoa
mbele ya Bwana Somi ... na baada ya tafakuri ya muda ... mashahidi hawa
waliachiwa.”
Mbele ya
Afisa Uchunguzi Somi, mashahidi hawa wawili, Hakimu Mkazi Msumi na Hakimu Mkuu
wa Wilaya Mlay, walikuwa wamesema kwamba “... huko nyuma (Bwana Msumi) aliwahi
kuitwa na mlalamikiwa baada ya wadhamini walioshindwa kukidhi masharti ya
dhamana ... kumpelekea malalamiko ya kukataliwa dhamana, maelezo ambayo hayakuwa
na ukweli wowote.” Aidha, kwa mujibu wa Afisa Uchunguzi Somi, “... katika hali
isiyokuwa ya kawaida Bw. Mlay, PDM hakuwa tayari kueleza kilichomsibu hadi
kujiengua katika usikilizaji wa kesi ambayo Bi. Mushi alidai ilikuwa inamkabili
rafiki yake wa karibu na Bi. Khaday.” Investigation Officer Karua hakuona
sababu yoyote ya kufuatilia ushahidi wa mahakimu hawa wawili!
Nne,
Investigation Officer Karua anakubali kwamba hali ilikuwa tete katika Kituo cha
Arusha: “Inaelekea mtuhumiwa alikuwa na mahusiano mabaya na baadhi ya
mahakimu.” Kama hivyo ndivyo ilivyokuwa, Investigation Officer Karua alikuwa na
wajibu wa kuchunguza chanzo cha mahusiano hayo mabaya, hasa kwa vile kulikuwa
sio tu na tuhuma bali pia ushahidi wa mahakimu husika kwamba Bi. Khaday alikuwa
anawaingilia mahakimu katika kazi zao. Hakufanya hivyo. Badala yake Taarifa ya
Investigation Officer Karua inaonekana kama jitihada za kumkosha Bi. Khaday
dhidi ya tuhuma nzito za ukosefu wa maadili ya kimahakama. Jitihada hizi
zilifanikiwa kwani miaka miwili baada ya Taarifa ya Investigation Officer
Karua, Bi. Khaday aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Na wala
siyo Bi. Khaday pekee aliyeneemeka na taarifa hiyo. Bi. Patricia Fikirini,
ambaye Taarifa ya Afisa Uchunguzi Somi inamwelezea kama mmoja wa mahakimu
waliosikiliza kesi ya mfanyabiashara maarufu wa Arusha, Justin Nyari iliyokuwa
chanzo cha tuhuma dhidi ya Bi. Khaday – alihusishwa na tuhuma dhidi ya Bi.
Khaday kwa maneno yafuatayo: “... Kama mtawala ... (Bi. Khaday) ... alisema
aliwahi, tena kwa nia njema, kumweleza Bi. Fikirini ... kuhusu uvumi kwamba
mume wake alikwenda gerezani na kuchukua mamilioni ya fedha kwa Bw. Nyari na
hivyo kumshauri awe mwangalifu zaidi”! Katika uteuzi wa majaji uliofanywa na
Rais Kikwete mwezi Juni mwaka huu, Bi. Patricia Fikirini naye ameteuliwa kuwa
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Wapo
wanaoweza kusema kwamba Bi. Khaday hakupatikana na hatia yoyote na kwa hiyo
haikuwa makosa kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Aidha, inaweza kudaiwa
kwamba Bi. Fikirini hajawahi kutuhumiwa kwa kosa lolote la maadili na kwamba
‘uvumi’ pekee hautoshi kumnyima mtu mwenye sifa haki ya kuteuliwa Jaji wa
Mahakama Kuu. Kwa wenye hoja za aina hii jibu langu ni kwamba kiwango cha ‘sifa
maalum’ kinachotakiwa na Katiba kwa mtu kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ni
mtu ambaye “... kwa kila hali anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama
Kuu....” Kiwango hiki ni cha juu kiasi kwamba kutokuwa na hatia pekee haitoshi
kumfanya mhusika kuwa ‘kwa kila hali anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa
Mahakama Kuu.’ Kwa maoni yangu, mtu aliyeundiwa uchunguzi wa kimaadili au
ambaye kuna uvumi unaomhusisha na rushwa ‘hafai kwa kila hali’ kukabidhiwa
madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu. Majaji Khaday na Fikirini wapo kwenye kundi
hili.
JAJI
ALOYSIUS MUJULIZI
Jaji
Aloysius Mujulizi alikuwa miongoni mwa watu ishirini walioteuliwa Majaji wa
Mahakama Kuu mwezi Februari, 2006. Kabla ya uteuzi wake, Jaji Mujulizi alikuwa
wakili wa kujitegemea katika kampuni ya mawakili ya Ishengoma, Masha, Magai
& Mujulizi Advocates (IMMMA) ya Dar es Salaam. Kampuni hii ya mawakili
ndiyo iliyoshiriki katika kuanzishwa kwa kampuni iitwayo Deep Green Finance Co.
Ltd. mnamo tarehe 18 Machi 2004. IMMMA Advocates vile vile walikuwa mawakili wa
Tangold Ltd.
Makampuni
haya mawili yanatuhumiwa kutumika kupitishia mabilioni ya fedha zilizoibiwa
Benki Kuu ya Tanzania kati ya mwaka 2005 na 2006. Kwa mfano, katika kipindi
kifupi cha miezi minne kati ya Agosti 1 na Desemba 10, 2005 kampuni ya Deep
Green Finance ilipokea jumla ya shilingi 10,484,005,815.39 kutoka akaunti ya
kulipia madeni ya nje (EPA) iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania. Katika kipindi
hicho hicho, kampuni ya Tangold Ltd. ililipwa dola za Marekani 13,736,628.73
kutoka kwenye akaunti hiyo ya EPA. Nyaraka zilizowasilishwa BRELA na mawakili
wa IMMMA Advocates na kusainiwa na Gavana wa Benki Kuu wa wakati huo Daudi
Ballali tarehe 20 Mei 2005 zinaonyesha kwamba Tangold Limited ilikuwa kampuni
ya kigeni kutoka Jamhuri ya Mauritius. Haya yote yalitokea wakati Jaji Mujulizi
akiwa wakili mwenza wa IMMMA Advocates.
‘SIFA
MAALUM’ ZENYE SHAKA
JAJI WA
RUFAA MBAROUK SALIM MBAROUK
Mbarouk
Salim Mbarouk aliteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania
mwaka 2008. Kabla ya uteuzi huo Jaji Mbarouk alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya
Zanzibar. Sifa za mtu kuteuliwa kuwa Jaji wa Rufaa zimeainishwa katika ibara ya
118(3) ya Katiba: “Majaji ... wa Rufani watateuliwa na Rais, kwa kushauriana na
Jaji Mkuu, kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kuteuliwa kuwa Majaji wa
Mahakama Kuu ... zilizoainishwa katika Ibara ya 109 ya Katiba au kutoka
miongoni mwa watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar
kwa mujibu wa sheria zinazotumika Zanzibar na wamekuwa na sifa hizo kwa muda
usiopungua miaka kumi na tano.”
Kwa
mujibu wa Ibara ya 94(3) ya Katiba ya Zanzibar, 1984, “mtu hatoweza kuteuliwa
kuwa Jaji au Kaimu Jaji wa Mahkama Kuu mpaka awe na shahada ya Sheria ya Chuo
Kikuu kinachotambuliwa au Chuo cha aina hiyo; au awe au amewahi kuwa Jaji wa
Mahkama zilizofanana na hii kwa kesi zote za jinai na madai katika Tanzania au
sehemu yoyote ya Jumuiya ya Madola au Mahkama ya Rufaa kutoka Mahkama hizo; au
awe Mwanasheria wa Zanzibar au Tanzania kwa kipindi kisichopungua miaka saba;
au awe na uzoefu wa Jaji au mwanasheria kwa pamoja usiopungua miaka saba.” Jaji
Mbarouk hajatimiza hata moja ya masharti hayo ya Katiba ya Zanzibar. Jaji huyu
hana shahada yoyote ya sheria inayotambuliwa na mamlaka ya ithibati ya Tanzania
kama inavyotakiwa na Ibara ya 109(7) ya Katiba. Jaji huyu ana stashahada ya juu
ya sheria (Post Graduate Diploma in Law) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
Shahada ya Uzamili ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha nchini Uingereza.
Uteuzi wa
Jaji Mbarouk kuwa Jaji wa Rufaa ulileta minong’ono mingi katika taaluma ya
sheria kiasi kwamba marehemu Wakili Leopold Kalunga anasemekana kufungua shauri
katika Mahakama Kuu ya Tanzania kutaka uteuzi huo utenguliwe. Hata hivyo,
Wakili Kalunga alifariki kabla ya shauri lake kusikilizwa na kwa hiyo
liliondolewa mahakamani. Aidha, monong’ono hiyo ilimfanya Jaji wa Rufaa Mbarouk
kujiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambako bado ni mwanafunzi hadi
ninapoandika Addendum hii.
MAJAJI
‘WALIOTOLEWA MITAANI’
Katika
Maoni ya Kambi tulidai kwamba “... sasa watu wanateuliwa kuwa Majaji wa
Mahakama Kuu ambao hawajawahi kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na -
kwa sababu hiyo - hawajafanyiwa vetting yoyote na mamlaka hiyo ya kikatiba....”
Ukiacha uteuzi wa Jaji wa Rufaa Mbarouk ambao haubanwi na masharti ya Ibara ya
109(1) na 113(1)(a) ya Katiba, majaji wengine waliotajwa kwenye Addendum hii
hawakupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama. Majaji wengine ambao pia
hawajawahi kupendekezwa na Tume hiyo ni pamoja Fatuma Massengi, Mary Sumari,
Imani Mkwawa-Aboud na Sekela Mushi.
No comments:
Post a Comment