Mkurugenzi wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Obeid
Mbangwa na wenzake wawili, wamefukuzwa kazi kwa kashfa ya kutorosha
wanyama hai 136 wa aina 14 tofauti kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Kilimanjaro (Kia), usiku wa Novemba 26, 2010.
Hatua hiyo
imefikiwa baada ya tume mbili zilizoundwa kuchunguza suala hilo bila
kuhusisha wizara yenyewe, kumaliza kazi yake na kukabidhi ripoti kwa
Waziri.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki
alisema jana mjini Dodoma kuwa mbali na watuhumiwa hao, mtumishi
mwingine wa wizara hiyo amevuliwa madaraka, wawili wamepewa onyo kali la
maandishi na wawili uchunguzi dhidi yao unaendelea.
Mbangwa
wakati wa kashfa hiyo ya kusafirisha wanyama hai wanaokadiriwa kuwa na
thamani ya Sh170 milioni kwa ndege ya kijeshi ya Qatar, alikuwa
Mkurugenzi Msaidizi Matumizi ya Wanyamapori.
Wengine waliotimuliwa
kazi ni Simon Gwera na Frank Mremi waliokuwa Maofisa Uwindaji wa
Kitalii, Cites na Utalii wa Picha mkoani Arusha.
Mkurugenzi
Msaidizi, Uendelezaji Wanyamapori, Boneventura Midala amevuliwa madaraka
kutokana na kutochukua hatua kikamilifu za ulinzi ambazo zingeweza
kuzuia kutokea kwa utoroshaji wa wanyama. Wakati wa tukio hilo alikuwa
Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Kuzuia Ujangili.
Katika hatua
hizo, maofisa wanyamapori daraja la pili, wawili waliotekeleza maelekezo
ya wakuu wao wa kazi yaliyo kinyume cha sheria wamepewa onyo kali la
maandishi.
Kagasheki aliwataja maofisa hao kuwa ni Ofisa Leseni
ya Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Arusha, Martha Msemo na
Ofisa Leseni Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Dar
es Salaam, Anthonia Anthony.
Rungu la wizara hiyo pia
limemwangukia Mkuu wa Kituo cha Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa
Picha Arusha, Silvanus Ukudo aliyepewa onyo kali la maandishi kwa
kushindwa kufuatilia kupata maelekezo ya Mkurugenzi wa Wanyamapori
kuhusu mtumishi wake aliyekiuka sheria katika utoaji wa vibali.
Ukudo
pia ameonywa kwa kushindwa kupeleka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, taarifa kuhusu mtumishi huyo ili achukuliwe hatua
za kinidhamu.
Kagasheki alisema uchunguzi unaendelea dhidi ya
watumishi wengine wawili, Ofisa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori,
Mohamed Madehele na Ofisa wa Kituo cha Uwindaji wa Kitalii, Cites na
Utalii wa Picha Arusha, Mariam Nyallu.
No comments:
Post a Comment