Friday, July 20, 2012

MADIWANI TEMEKE KUJENGA SHULE ZA MAGOROFA


Madiwani wa Manispaa ya Temeke Dar es Salaam wameitaka serikali kujenga shule za ghorofa kufuatia ufinyu wa nafasi katika shule za kata ambazo zinaongezewa madarasa kila mwaka.

Hayo yalisemwa na Diwani wa Kurasini Bw. Wilfred Kimati jana walipokuwa wakikagua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa mwaka wa fedha 2011/2012  walipotembelea ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya sekondari ya Keko iliyopo Temeke yaliyoghalimu milioni 34.


Bw. Kimati alisema kuwa kama serikali ikiendelea kujenga majengo ya kawaida itasababisha wanafunzi kukosa maeneo ya michezo pamoja na nafasi kuwa finyu.

Kwa mujibu wa Mchumi wa manispaa hiyo Bw. David Mgonja alisema kuwa sekondari hiyo imekuwa ikiongezewa madarasa mawili kila mwaka ili kuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wengi.

Hata hivyo madiwani hao baada ya kutembelea shule ya sekondari ya Pendamoyo kukagua ujenzi wa madarasa matatu yaliyogharimu milioni 69 walipendekeza kuwa mazingira ya shule yaboreshwe ikiwa ni pamoja na kupanda miti ili kutunza mazingira.

Kwa upande mwingine madiwani hao walipendekeza jengo la kuagia maiti katika hospitali ya Temeke liboreshwe ikiwa ni pamoja na kuweka viti vya kumpumzikia.

wakati huo huo mfanyakazi wa kuhudumia maiti katika hospitali hiyo Bw. Gervas Gerazius aliwaeleza madiwani kuwa muntuari hiyo imezidiwa kufuatia kuwa na maiti wengi kwa siku.

Bw. Gerazius aliwaeleza madiwani kuwa uwezo wa montuali hiyo ni maiti 15 ambapo huwa zinazidi kila siku huku baadhi ya maiti ambazo zinazopelekwa na polisi hukaa kwa muda mrefu.

"Kuna maiti imeletwa na polisi hapa ambapo leo ina siku ya 19 huku nyingine zikitakiwa kupata huduma ya kuifadhiwa," alisema Bw. Gerazius

Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni pamoja na madarasa ya shule ya sekondari Keko, sekondari ya Pendamoyo, ujenzi wa zahanati Yombo, Ujenzi wa barabara shule ya msingi Kilakala Yombo, Ujenzi wa mfereji barabara ya Evereth, Ujenzi wa jengo la kuagia maiti pamoja na ujenzi wa mabanda ya soko la Temeke Stereo.

No comments:

Post a Comment