Thursday, August 2, 2012

CLINTON ATAKA AFRIKA KUJENGA DEMOKRASIA



Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton amezitaka serikali za Afrika kuimarisha demokrasia huku akisifia maendeleo ya kiuchumi yaliyofikiwa barani humo.

Akizungumza katika chuo kikuu cha Senegal mjini Dakar, Bi Clinton amesema kumekuwepo na matukio ya kuogofya barani humo, ikiwa ni pamoja na kitisho cha wapiganaji wa Kiislam katika eneo la Sahel na kuongezeka kwa biashara ya usafirishaji wa dawa za kulevya nchini Guinea- Bissau.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani Hillary Clinton (kulia) akikutana na rais wa Senegal Macky Sall katika ikulu mjini Dakar Agosti 1, 2012

Mwandishi wa BBC, Thomas Fessy amesema Bi Hillary Clinton amelisifu taifa la Senegal kwa kudumisha kiwango cha juu cha demokrasia, akisema angependa kuona mataifa mengi katika eneo hilo yakiiiga mfano huo.

Pamoja na hayo Bi Clinton aliongeza kuwa kuna mataifa mengi barani Africa ambayo bado yana viongozi wa kidikteta ambao hujali tu kuhusu jinsi ya watakavyobakia madarakani kuliko kufikiria maslahi ya raia wao.

Bi Clinton hata hivyo alisema kuwa taifa la Marekani halitaendelea tena kutoa msaada kwa serikali ya Mali hadi pale viongozi wa kijeshi watakapo kubali kurejeshwa kwa utawala wa kiraia na viongozi kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.

Vile vile amelionya taifa la Guinea Bissau kuhusu kuendelea kuwategemea wafanyibiashara wa dawa za kulevya kutoka Amerika ya kati. Na Kuhusu ukosefu wa ajira kwa vijana katika mataifa mengi barani Africa, Bi Clinton alisema kuwa viongozi wa Africa wanafaa kuwaheshimu raia wake ili kuzuia mapigano yanoyotokana na hasira.

No comments:

Post a Comment