CHAMA cha Walimu Tanzania
(CWT), kimejivunia mafanikio ya mgomo waliouitisha wakidai umefanikiwa
kwa asilimia 95.7 na kutangaza mpango wa kuzidisha mapambano hadi
kieleweke.
Pia chama hicho kimeitaka Serikali kuacha vitisho kwa
walimu ambao wameunga mkono mgomo huo na kudai kuwa, vitisho hivyo
havitasaidia kupatikana muafaka.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es
Salaam jana, Rais wa chama hicho, Bw. Gratian Mukoba, alisema kila siku
walimu wazidi kuunga mkono mgomo huo kwa kuwa ni halali na hawahitaji
kumsikiliza mtu mwingine zaidi ya CWT.
Alisema mgomo ulipoanza
Jumatatu wiki hii, uliungwa na walimu kwa asilimia 90, lakini siku
zinavyozidi kwenda idadi inaongezeka na kuwataka walimu waendelee
kushirikiana ili wapate haki zao ili waweze kutoa elimu bora si bora
elimu.
“Walimu wanatakiwa kushiriki mgomo kikamilifu kwani upo
kihalali kwa mujibu wa katiba ya nchi na ile ya chama chetu, kimsingi
walimu wasioshiriki mgomo huu ni wanafiki na wanajipendekeza ili wapate
vyeo vya upendeleo,” alisema.
Alidai kushangazwa na hatua ya
Serikali na Bunge kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kutangazia umma kuwa
mgomo wa walimu ni batili, huku Bunge kupitia Naibu Spika, Bw. Job
Ndugai, akidai Mahakama ingetoa hukumu Julai 31 mwaka huu, saa saba
mchana, wakati pande zote mbili zilikuwa hazijasikilizwa.
Alisema
CWT imepokea taarifa ya kukamatwa kwa baadhi ya walimu katika Wilaya za
Tarime, Rungwe, Kyela, Babati, Pwani, Morogoro na Ruvuma.
Bw.
Mukoba alisema maeneo mengine watendaji wa CWT wanatishwa na wakuu wa
mikoa pamoja na Kamati za Ulinzi za Mikoa ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam.
“Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Mecky Sadick amewatishia wanachama na
viongozi wa chama na kuamuru wakamatwe, sisi tunasema mwajiri wetu si
Mkuu wa Mkoa wala Wilaya, tunazidisha mapambano yetu hadi kieleweke,”
alisema Bw. Mkoba.
Aliongeza kuwa, kuna uvumi unaodai kuwa
wanafunzi wanaofanya maandamano wamefundishwa na walimu jambo ambalo si
kweli na kuitaka Serikali kukaa mezani na CWT kwani viongozi wake wapo
tayari ili kutafuta muafaka wa mgogoro huo.
Wilaya ya Kyera
Kutoka
Kyera, mkoani Mbeya, Mwandishi Wetu ameripoti kuwa, Katibu wa CWT
wilayani humo, Bw. Pastori Mangula, amefikishwa katika Mahakama ya
Wilaya kwa kosa la kushawishi walimu kuingia kwenye mgomo ambao umeanza
juzi.
Akisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Joseph Luambano,
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Bw. Nicholaus Charles, alisema mshtakiwa
anakabiliwa kosa la kushawishi walimu wa shule tatu za msingi mjini
Kyela kuingia kwenye mgomo lakini alipewa dhamana ambapo kesi hiyo
itatajwa tena Agosti 28 mwaka huu.
Dar es Salaam
Uchunguzi
uliofanywa na Majira jana, ulibaini baadhi ya madarasa katika shule
mbalimbali jijini Dar es Salaam, yalifunguliwa lakini hakukuwa na
wanafunzi shuleni wengi wao wakiwa mitaani.
Hali hiyo ilijitokeza
katika Shule za Msingi Kijichi, Bwawani, Mbagala Kuu, na Maendeleo
zilizopo Kata ya Kijichi na Mbagala Kuu, wilayani Temeke.
Katika
shule zingine kama Lumumba iliyopo katikati ya jiji, walimu walionekana
madarasani wakiwa wamekaa na wengine walikuwa ofisini na ubao wa ofisi
uliandikwa maneno yaliyowataka walimu kudumisha mshikamano.
Maandishi
hayo yalisomeka “Solidarity Forever, Solidarity for Changes, No
Returning Back”, huku ofisi ya Mwalimu Mkuu ikiwa imefungwa lakini
walimu hao walikataa kuzungumza na waandishi.
Mkoa wa Singida
Mkoani
Singida, wazazi na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, wametoa
wito kwa walimu kuacha kuendelea na mgomo ili kuepusha athari zinazoweza
kujitokeza.
Ushauri huo ulitolewa jana wakati wazazi hao
wakizungumzia athari za mgomo huo ambapo katika baadhi ya shule mkoani
humo, baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba walionekana wakifundishana
wenyewe bila msaada wa mwalimu.
Mwenyekiti wa CWT Mkoa humo, Bw.
Darran Jumbe, alisema CWT kimetoa maelekezo kwa walimu wote waendele na
mgomo hadi Serikali itakapowatimizia madai yao.
Kwa upande wake,
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Bi. Salome Singano, alisema
walimu 573 ndio wameunga mkono mgomo huo na wengine 67 wanaendelea na
kazi.
Wilaya ya Hai
Katika Wilaya ya Hai, mkoani
Kilimanjaro, imeripotiwa walimu wameanza kupata vitisho baada ya kuanza
kupita Waratibu wa Elimu Kata na Wilaya na kushinikizwa wajaze fomu
zenye vipengele vitatu kikiwemo cha kukubali au kukana kushiriki mgomo.
Walimu waliozungumza na Majira kwa sharti la kutotajwa majina yao, walidai kinachofanyika sasa ni kupewa vitisho.
Habari hii imeandikwa na Rehema Maigala, Israel Mwaisaka, David John, Salim Nyomolelo na Damiano Mkumbo.
source: gazeti la majira
No comments:
Post a Comment