Thursday, August 2, 2012

MCT WAPINGA KUSIMAMISHWA MWANAHALISI

BARAZA la Habari Tanzania (MCT), limedai kusikitishwa na taarifa za kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi bila kikomo na kusisitiza kuwa, uamuzi huo hawauungi mkono.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Katibu Mkuu wa MCT, Bw. Kajubi Mukajanga, imesema siku zote wanaamini makosa na matatizo ya kitaaluma hayawezi kumalizwa kwa kufungia magazeti au chombo kingine cha habari.


Alisema kuanzishwa MCT, kunadhihirisha wazi kuwa vyombo vya habari vinaweza kufanya makosa au kutofautiana na wadau wake ndio maana katika kipindi chote cha uwepo wake, wamekuwa wakishughulikia malalamiko dhidi ya makosa ya kitaaluma.

“Kufunga au kusimamisha vyombo vya habari ni ukikwaji wa uhuru wa vyombo hivyo na kuwanyima wateja wa chombo hicho haki ya kupata habari za chaguo lao, pia kinawanyima raia ambao wamekuwa wakitumia chombo hicho haki ya kueleza maoni yao,” alisema Bw. Mukajanga.

Aliongeza kuwa, Serikali imechagua kutumia sheria ambayo  kila mdau wa habari anaiona mbaya na kuilalamikia ambapo matatizo ya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, yapo ya aina tatu.

Kwanza sheria hiyo inaweza kutumiwa bila kujali haki kwani inampa Waziri wa Habari uwezo wa kusimamisha gazeti wakati wowote kadiri anavyojisikia, pili inakiuka haki za asili zinazompa mtu haki ya kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa.

“Kukiukwa kwa haki ya kusikilizwa ni ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu zilizomo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano 1977 na tatu sheria haitoi haki ya kukata rufaa kwenye ngazi za juu,” alisema.

Bw. Mukajanga aliwataka Wahariri kuzingatia maadili ya taaluma na kuongeza kuwa, hakuna ulinzi mkubwa dhidi ya amri mbovu za watawala kuliko kuzingatia maadili ya kitaaluma.

Alisema kushindwa kuzingatia maadili kunawapa mwanya wanaopenda kutumiwa kwa sheria mbaya na kuzuia kutungwa Sheria Mpya zilizo rafiki na zinazotoa uhuru kwa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.

source:gazeti la majira

No comments:

Post a Comment