Tuesday, July 3, 2012

WANACHI WAJITOKEZA KUTOA MAONI-KATIBA

TUME ya kukusanya maoni ya mabadiliko ya uundawaji wa Katiba Mpya imeanza kukusanya maoni yake katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ambapo wananchi mbalimbali wameonesha moyo wa kutoa maoni.

Wananchi waliohudhuria kutoa maoni yao walianza kwa kumtaka Mwenyekiti wa Aerikali ya Mtaa wa Majengo wilayani hapa aondoke katika meza ya wajumbe wa kamati ya taifa ya maoni.


Mwenyekiti huyo Bw. Noel Mseveni ambaye alikuwa katika meza ya Kamati ya  Tume ya kupokea maoni kama mwenyeji na aliyekuwa na kazi ya kuruhusu kila mwananchi anayenyoosha mkono kutoa maoni, wananchi hao walimtuhumu aondoke katika safu hiyo kwa madai ya kupendelea.

Wananchi hao waliwataka wajumbe wa tume hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wa msafara wilayani hapa Bi. Maria Kashonda na Bw. Abubakari  Ally kuamua akae pembeni Bw. Mseveni.

Wakitoa maoni yao wananchi wa Mjini Kahama walisema, Katiba Mpya ijayo lazima ipunguziwe madaraka na mawaziri wasiwe wabunge bali wateuliwe na kuthibitishwa kupitia Bunge.

Pia wananchi hao walisema, nafasi za wakuu wa wilaya zifutwe huku wakuu wa mikoa badala ya kuteuliwa wawe wanachaguliwa.

Wananchi hao, waliokuwa wamehamasika walisema pia Katiba Mpya iweke wazi Baraza la Mawaziri huku wakipinga suala la Mahakama ya Kadhi lisiwekwe katika katiba hiyo.

Walisema katika katiba hiyo Muungano uendelee kuwepo bila kumkwaza mtu yeyote katika pande hizo na serikali mbili huku wengine wakitaka serikali ziwe tatu.

source:majira.co.tz

No comments:

Post a Comment