JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia mkazi wa Kijiji cha
Likarangiro, Kata ya Tanga, wilayani Songea, Bw. Batazari Shawa, kwa
kosa la kumchapa zaidi ya saa tatu na kumjeruhi mtoto wa kambo (jina
tunalo), baada ya kupoteza sh. 800, zilizotokana na mauzo ya mahindi.
Akizungumza na Majira nje ya Kituo Kikuu cha Polisi mjini Songea, mama
mzazi wa mtoto huyo, Bi. Scolastika Njafura (38), alisema mtoto huyo
alipata maumivu baada ya kuchanika katika makalio.
Bi. Njafura alisema siku ya tukio, alirejea kutoka shambani na kumkuta
mtoto wake akiwa amelala lakini alikuwa akilia kutokana na maumivu
aliyokuwa nayo.
“Nilipomuuliza kulikoni alisema, baba yake wa kambo amempiga viboko
baada ya kupoteza sh.800, zilizotokana na mahindi aliyouza hapa kijijini
na kunionesha majeraha ya vidonda kwenye makalio.
“Vidonda hivi vilimfanya ashindwe kusimama na kutembea hivyo
nimelazimika kuja polisi kuomba PF3 ya kwenda hospitali kwa ajili ya
matibabu kabla ya kufungua jarada SO/IR/2618/2012 na mtuhumiwa
amekamatwa,” alisema.
Kwa upande wake, mtoto aliyefanyiwa kitendo hicho alisema baba yake ya
kambo ana tabia ya kuwafanyia yeye na wagodo zake hasa mama yao
anapokwenda shambani kwa kuwacharaza viboko akidai wanamdharau na
hawamuheshimu jambo ambalo si kweli.
“Siku ya tukio baada ya kula chakula cha mchana, baba alinituma kwenda
kuuza mahindi kwa walanguzi, baada ya kufika yalipimwa na thamani yake
ilikuwa sh. 800.
“Wakati narudi nyumbani nilikuwa ninikimbia ili niweze kuwahi, baada ya
kufika na kuangalia fedha niliyopewa sikuiona hivyo nilibaini zimepotea
wakati nakimbia ili kuwahi nyumbani.
“Baada ya kumweleza baba mazingira halisi yaliyochangia nipoteze fedha
hizi, kwanza alibadilika sura, kuchukua fimbo ya mti wa mwanzi na kuanza
kunichapa hadi kusababisha nikose nguvu,” alisema mtoto huyo.
Kwa upande wake, Bw. Shawa ambaye anatuhumiwa kufanya kitendo hicho, alikiri kumchapa mtoto huyo zaidi ya saa tatu.
Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake mkoani hapa, Inspekta Anna
Tembo, aliitaja jamii inayolea watoto ambao wameondokewa na wazazi wote
au mmoja, kutoa matunzo mazuri kwa watoto hao badala ya kuwafanyia
vitendo vya ukatili, kuishia katika mikono ya dora na hatimaye gerezani
kutumikia kifungo.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Deusdedit Nsemeki,
alikiri kupokea taarifa ya mtoto huyo ambaye anadaiwa kufanyiwa vitendo
vya kikatili.
source : majira.co.tz
No comments:
Post a Comment