BARAZA la Madaktari Tanganyika limewafutia usajili madaktari wote waliokuwa
katika mafunzo ya vitendo (Internship), baada ya kupatikana na hatia ya
kufanya mgomo wakiwa kazini.Taarifa ya Baraza hilo iliyotolewa Dar es Salaam
jana imeeleza kuwa madaktari 319 wamepoteza sifa ya kuendelea na taaluma hiyo
hivyo usajili wao umesitishwa rasmi kuanzia jana.Mwenyekiti wa Baraza hilo,
Dk Donan Mmbando amewataka madaktari hao kurudisha hati zao za usajili wa
muda kwenye Ofisi ya Msajili wa Madaktari.
“Kwa kuzingatia masharti ya sheria kuhusu kupata usajili wa muda, Baraza la
Madaktari Tanganyika limeridhia kwamba madaktari wote ambao walijihusisha na
mgomo, wamepoteza sifa na kwa sababu hiyo usajili wao umesitishwa kuanzia
tarehe 11 Julai, 2012.”
“Madaktari wote wanaohusika wanatakiwa kurejesha hati za usajili wa muda
kwenye Ofisi ya Msajili wa Madaktari kabla ya terehe 17 Julai, 2012.”
Dk Mmbando alisema, awali Baraza hilo lilipokea malalamiko kutoka kwa Katibu
Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwamba baadhi ya madaktari waliopata
usajili wa muda ili kuwawezesha kufanya mafunzo kwa vitendo (Internship),
waligoma kutoa huduma kwa wagonjwa kwa kati ya Juni 23 na Juni 29 mwaka huu.
Alisema madaktari hao walipangiwa kutoa huduma katika Hospitali za Muhimbili,
KCMC, Rufaa Mbeya, Sekou Toure na Bugando za Mwanza, Amana, Temeke na
Mwananyamala za Dar es Salaam, Haydom - Arusha, St Francis-Ifakara na Dodoma.
Alisema kutokana na mgomo huo, uongozi wa hospitali husika uliwaandikia barua
iliyomtaka kila daktari aliyeshiriki kwenye mgomo huo kuripoti kwa Katibu
Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.Dk Mmbando alisema kutokana na
malalamiko yaliyowasilishwa kwenye Baraza hilo, Msajili wa Baraza,
alimwandikia kila daktari aliyelalamikiwa Taarifa ya Kusudio la kufanya
Uchunguzi dhidi yake, juu ya malalamiko yaliyowasilishwa na Katibu Mkuu,
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Alisema baada ya kuyafanyia kazi malalamiko hayo, Baraza limebaini kuwa kwa
mujibu wa Kifungu cha 15(2) cha Sheria ya Madaktari, Sura ya 152, madaktari
waliokuwa kwenye mgomo na ambao kwa sasa wameondolewa katika hospitali
walizokuwa wakifanya mafunzo kwa vitendo, wamepoteza sifa za kupata usajili
wa muda.
Katibu wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania (MAT), Dk Edwin Chitage alisema
alikuwa hajapata rasmi taarifa hizo licha ya kusikia fununu... “Sijapata
taarifa rasmi lakini ni jambo tulilolitarajia na hatutashangaa tukisikia hilo
kwa sasa subiri nithibitishe halafu nitatoa msimamo wetu.”
Kiongozi wa madaktari kortini
Katika hatua nyingine, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala
Mkopi jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar
es Salaam, akikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kudharau amri ya
Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi ya kuwataka kusitisha mgomo kupitia vyombo vya
habari.
Amri hiyo ilitolewa Juni 22, mwaka huu na Jaji Sekela Moshi na kuwataka
madaktari kurejea kazini mara moja, lakini amri hiyo haikutekelezwa.
Jana, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka alimsomea Dk Mkopi hati ya
mashtaka na kumweleza Hakimu Faisal Kahamba kuwa kati ya Juni 26 na 28, mwaka
huu, Dk Mkopi akiwa Rais wa MAT, alidharau amri iliyotolewa na Mahakama
Kuu Kitengo cha Kazi Juni 26, mwaka huu ikimtaka kutoa tangazo kwa wanachama
wa chama hicho kupitia vyombo vya habari kwamba wasishiriki katika mgomo.
Kweka alidai kuwa Juni 27, mwaka huu Dk Mkopi aliwashawishi wanachama
kushiriki kufanya mgomo kitu ambacho ni kinyume na amri iliyotolewa Juni 26,
mwaka huu.
Hata hivyo, Dk Mkopi alikana mashtaka hayo na upande wa mashtaka ulidai kuwa
upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Kiongozi huyo wa madaktari yupo
nje kwa dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 8, mwaka huu
itakapotajwa na kuangaliwa kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.
Afya ya Dk Ulimboka
Wakati huo huo, afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven
Ulimboka imezidi kuimarika.
Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk Edwin Chitage alisema jana kwamba: “Tofauti na
ilivyokuwa mwanzo, kwa sasa afya yake imezidi kuimarika, anakula mwenyewe
lakini pia anazungumza mwenyewe na rafiki zake wa hapa nchini kwa njia
ya simu.”
Katika siku za karibuni, hali ya Dk Ulimboka ilielezwa kubadilika ghafla na
kulazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) kutokana matatizo
mbalimbali, yaliyotokana na kupigwa ikiwamo figo kushindwa kufanya kazi.
Alisafirishwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi Juni 28, mwaka huu kwa ushauri
uliotolewa na jopo la madaktari lililokuwa likimhudumia.
UN yanena
Katika hatua nyingine, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Dk
Alberic Kacou amepokea barua ya MAT kuomba ulinzi kwa Dk Ulimboka
anayeendelea na matibabu Afrika Kusini kwa madai kuna kikosi kilichotumwa
kuhakikisha harudi nchini akiwa hai.
Akizungumza jana Dar es Salaam jana, Dk Kacou alisema suala hilo la kutoa
ulinzi watalitoa baada ya kuwasiliana na wote waliohusishwa kwenye waraka wa
ombi hilo.
Mgomo wamalizika
Mgomo uliokuwa ukiendelea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya
Mifupa (Moi), Dar es Salaam umemalizika na huduma katika hospitali hizo
zimerejea kama kawaida jana.
Waandishi wa habari waliotembelea hospitali hizo waliona wagonjwa wakiwa
wanaendelea kupokewa na kupatiwa huduma kama ilivyokuwa awali, kabla ya mgomo
uliodumu kwa takriban majuma mawili yaliyopita |
No comments:
Post a Comment