Tuesday, July 10, 2012

VIONGOZI WA CHADEMA WABANWA


Baada ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuibuka na kudai kuibaini mikakati ya kutishiwa maisha na idara ya usalama wa Taifa ,kutokana na walichokitamka jana Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi ameliagiza Jeshi la Polisi kuwahoji viongozi hao ambao walidai kuwa mauaji hayo yamepangwa kufanywa kwa kuwekewa sumu kwenye chakula au kwa kutumiwa makundi ya ujambazi.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini, Dk Nchimbi alisema licha ya kudai kwamba wanatishiwa, ameshangazwa na msimamo wa viongozi hao kukataa kupeleka suala hilo polisi kwa madai ya kuhofia suala hilo halitafanyiwa kazi.

Alisema kwamba licha ya jeshi la polisi kusita kuwahoji viongozi hao kwa madai ya kutoaminika, lakini sasa ameliagiza liwahoji na kuzifanyia uchunguzi tuhuma zao
Alisisitiza kuwa watawahoji viongozi hao kwa sababu suala la usalama wa Mtanzania yeyote hivyo ni lazima polisi watimize wajibu wao na kama tuhuma hizo zitasibitishwa si za kweli watachukuliwa hatua kulingana na sheria za nchi

“Ni lazima tuwahoji ili tujue ni nani amewatisha na kwa sababu zipi. Hatutamuomba mtu ruhusa ya kumlinda kwa sababu huo ni wajibu na kazi yetu kuwalinda raia, hilo halina mjadala. Hatua zitachukuliwa endapo itabainika kuwa madai yao yana ukweli,” alisema Dk Nchimbi.

Aliwataka viongozi wote wa kisiasa wakiwamo wa Chadema wanapohisi kutishiwa usalama wao, watoe taarifa polisi ili vyombo vya dola viyafanyie uchunguzi malalamiko yao ili utaratibu ufanyike kuhusu usalama wao kama sheria inavyotaka.

Alionya tabia ya viongozi kuzungumza nje ya utaratibu akisema haikubaliki kwani inaweza kuwa ni mbinu za kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

Dk Nchimbi alisema jambo hilo si jema kwani linajenga hofu miongoni mwa Watanzania na kuwafanya wasiviamini vyombo vyao vinavyowalinda kwa mujibu wa sheria.
“Ni kweli kuwa kila mwanasiasa anataka kukubalika na umma lakini, akubalike katika taratibu zinazokubalika,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:

“Ingekuwa Serikali inataka kukubali umaarufu kama huo, basi ingetumia mwanya wa haohao Chadema wakati mitandao ya kijamii iliposambaza taarifa kuwa Chadema ilihusika na kifo cha marehemu, Chacha Wangwe.”

Alisema Serikali haikukurupuka na kuwakamata, badala yake ilifanya uchunguzi kwanza na matokeo yake alikamatwa dereva wake ambaye ameshachukuliwa hatua.
Alisema kama Serikali ingekuwa inatafuta umaarufu, ilikuwa ni fursa nzuri kwake kujipatia umaarufu na kukivuruga chama hicho kwa kuwakamata viongozi wa Chadema hasa baada ya kuwapo kwa uvumi kwamba wamemuua kiongozi huyo.

“Viongozi wetu wa kisiasa ni lazima wafanye mambo ambayo kesho na keshokutwa watakiri mchango wao, ama katika ujenzi au uharibifu wa nchi yetu. Kila siku wakilalamika kuwa wanataka kuuawa basi ni lazima watu watawashangaa kwani badala ya kutatua matatizo ya wananchi wanabaki wakilalama wanataka kuuawa. Watu kama hawa wanafanya hivi kwa masilahi yao, wanaweza kuwagombanisha wananchi.”

Waziri Nchimbi aliwataka wananchi na viongozi wa kisiasa kuondoa hofu kwani Serikali ina wajibu wa kuwalinda na hakuna mtu atakayenufaika kwa mauaji ya wanasiasa hao.


Kauli hizo za Serikali zinatokana na tuhuma za Chadema kwamba kimebaini njama za kuwaua viongozi wake hao waandamizi ambazo zinaratibiwa na kigogo mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa na kwamba nyendo zao zimekuwa zikifuatiliwa kwa saa 24.

Tuhuma hizo za Chadema zilitolewa juzi na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni akisema: “Sisi Chadema hatuna mambo ya siri tunayotaka kufanya katika nchi hii. Matatizo ya Watanzania yapo wazi na yanajulikana na kila mmoja, Serikali ya CCM itekeleze sera na ahadi zao kwa wananchi na si vitisho.”

No comments:

Post a Comment