Tuesday, July 10, 2012

DKT. MIGIRO AREJEA NCHINI


ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dkt. Asha-Rose Migiro, amerejea nchini jana na kuzungumzia suala la kuwania au kutowania nafasi ya urais mwaka 2015.

Dkt. Migiro aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam, saa tisa alasiri na kupata mapokezi makubwa yaliyoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano ya Kimataifa, Bw. Bernard Membe.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dkt. Migiro, alisema kwa sasa ni mapema kuzungumzia dhamira yake ya kuwania nafasi hiyo kwani tayari kuna Rais ambaye yupo madarakani.

“Kwa sasa ni mapema kuzungumzia suala la kuwania urais ila wakati ukifika naweza kulizungumzia,” alisema Dkt. Migoro, wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari.

Alisema hivi sasa ataripoti kazini kwa mwajiri wake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Sheria kwani alipoondoka kwenda New York, nchini  Marekani kutumikia wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu wa UN, aliomba likizo ya bila malipo.

“Kesho (leo), naenda kuripoti kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (Profesa Rwekaza Mkandara) ili aweze kunipangia kazi ya kufanya,” alisisitiza Dkt. Migiro.

Kuhusu uteuzi wake wa kufanyakazi UN, amesema Tanzania imepata heshima kubwa pamoja na kujulikana kimataifa.

“Nampongeza Rais Jakaya Kikwete, kwa kuongoza nchi katika misingi ya utawala bora eneo ambalo limechangia kuipatia sifa nyingi Tanzania nje ya nchi,” alisema.

Dkt. Migiro pia aligusia mchakato unaoendelea wa kukusanya maoni ya Katiba Mpya na kusema kuwa, utasaidia kuongoza nchi kikamilifu.
source:majira.co.tz

No comments:

Post a Comment