Tuesday, July 10, 2012

UNYAMA WA KUBAKA VIKONGWE-KAGERA

Ni unyama mkubwa kwa vikongwe – 2 *Kikongwe aliyebakwa apoteza fahamu *Wananchi waamua kuitisha mkutano

Na Mwandishi Wetu, Kagera

JANA gazeti hili liliandika habari iliyohusu vitendo vya kinyama wanavyofanyiwa wanawake wenye umri mkubwa (wazee), katika Kata ya Nshamba, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera.

Habari hiyo ilieleza kuwa, unyama wanaofanyiwa wanawake hao ni pamoja na kubakwa na vijana wenye umri mdogo na kuondolewa nyeti zao. Vitendo hivyo vinahusishwa na imani za kishirikiana.

Katika mwendelezo wa habari hiyo, Majira lilizungumza na mwathirika mwingine wa unyama huo Bi. Adrofina Anacleti (74), mkazi wa Kijiji cha Rutenge ambaye anakiri kubakwa na vijana wanaounda mtandao huo na kupoteza fahamu.

“Nilipoteza fahamu baada ya purukushani ya kutaka kujiokoa bila mafanikio, kwa kuwa nilikuwa nakaa peke yangu, nilimiomba mtoto wangu wa kiume aje tuishi wote.

“Jambo la kusikitisha, siku chache tangu mtoto wangu ahamie nyumbani kwangu kwa lengo la kunilinda, naye aliuawa kikatili na maiti yake kutupwa nje ya nyumba yake.

Akizungumza na Mwandishi wetu huku akitoa machozi, Bi. Anaclet, alionesha mlango waliotumia vijana hao kuingia ndani na kufanikisha azma yao ya kumbaka.

Alisema tangu afanyiwe unyama huo, hapati usingizi sawasawa na  inapofika saa nane usiku lazima aamke.

Kutokana na taarifa za ukatili kwa vikongwe wilayani humo, Majira lilimtafuta Mkuu wa Kituo cha Polisi Nshamba, Bw. Nashon Simon, ili kupata maelezo ya kina juu ya unyama huo.

Pamoja na kutoa sharti la kutorekodiwa, alimtaka Mwandishi wetu akamuone Mkuu wa Polisi wilayani humo (OCD), lakini alikiri kuwa na taarifa za vitendo hivyo.

“Sina hakika kama vikongwe hawa wanafanyiwa vitendo vya ubakati, mambo haya yanahusishwa na migogoro ya kifamilia,” alisema Bw. Simon.

Hata hivyo, ushirikiano wake kwa Mwandishi wetu ulikuwa mdogo kwa madai kuwa, yeye si msemaji wa polisi. Wakazi wa Kijiji cha Rutenge, waliitisha mkutano wa kijiji ili kujadili jinsi ya kuvikabili vitendo hivyo.

Mkutano huo ulifanyika Juni 14 mwaka huu, Mkuu wa Kituo cha Polisi wa Nshamba (OCS), Bw. Simon, ndiye aliyekuwa Msemaji Mkuu katika mkutano huo.

Mambo yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na vitendo vya ubakaji kwa vikongwe, kunyang'anywa mashamba yao na imani za kishirikina ambapo baada ya maongozi ya muda mrefu, wanakijiji hao walifikia makubaliano ya pamoja.

Makubaliano hayo ni pamoja na baa zote kufunguliwa saa 10 jioni hadi saa tatu usiku zaidi ya hapo hatua kali kuchukuliwa na kuacha tabia ya kuficha siri za waarifu jambo ambalo lilizua mjadala mkubwa katika mkutano huo.

Vikongwe hao walimuomba Bw. Simon kuhakikisha mtu yeyote ambaye ni mkazi wa kata hiyo ambaye amefungwa na kumaliza kifungo chake, apewe barua ya kuonesha katika Serikali ya kijiji kuwa amemaliza chake hivyo ni mtu mwema.

Hali hiyo inatokana na wananchi kukosa imani na Jeshi la Polisi kuwaachia waarifu bila kuwa na taarifa yoyote hivyo kuendelea kuwa tishio kwa jamii.

“Tunahitaji vitamburisho maalumu kwa washtakiwa wanaomaliza kutumikia vifungo vyao gerezani,” walisema vikongwe hao.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nshamba, Bw. Martin Rutaiwa, alikiri kuwa na taaarifa za unyama huo kwa vikonge na kudai kuwa, wananchi hawana ushirikiano mzuri kwa kushindwa kuwataja wahusika wa vitendo hivyo.

Alipoulizwa kuhusu uwepo wa kundi la watu ambao wanahusika kufanya vitendo hivyo Bw. Rutaiwa alikiri kupambana na kundi hilo hata kujeruhiwa.

“Nasikitika kusema kuwa, watu wanaofanyiwa vitendo hivi vya kinyama hawana ushirikiano, mimi namfahamu bwana (jina tunalo), kwa jina lingine anaitwa...ambaye nimewahi kupambana naye mara kadhaa.

“Huyu bwana amekuwa tishio kubwa lakini hawezi kufunguliwa kesi bila kuwepo walalamikaji, mimi nawashangaa wananchi, hivi kweli huyu jamaa anaweza kuua kila mtu, wajitokeze ili sheria iweze kuchukua mkondo wake,” alisema Bw. Rutaiwa.

Kwa upande wake OCD wa Wilaya ya Muleba, Bw. Pascal Nkuba, alipotafutwa ili kuthibitisha taarifa hizo, alidai yeye ni mgeni tangu ahamishiwe wilayani humo.

“Mimi hapa nina wiki moja tu, sina taarifa zozote juu ya mambo haya labda nifuatilie kwa sababu umenipa taarifa hizi, lakini mimi sio mzungumzaji wa polisi kamuone RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa)”, alisema Bw. Nkuba.

Majira lilipomtafuta RPC kwa njia ya simu, na kumueleza juu ya vitendo wanavyofanyiwa vikongwe hao katika Wilaya ya Muleba, alisema yeye hawezi kuzungumza na mtu asiyemjua.

“Kama unataka taarifa zozote nenda kituo chochote cha polisi uoneshe kitambulisho chako kisha wanipigie hata huko Dar es Salaam, unaweza kufanya hivyo,” alisema.

source:majira.co.tz

No comments:

Post a Comment