Wednesday, August 8, 2012

SEHEMU YA HOTUBA YA WAZIRI MEMBE-KUHUSU MALAWI NA TANZANIA-BUNGENI


Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukishuhudia mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii duniani kote ambayo wakati mwingine yanahitaji nchi kuonesha msimamo wake kwa baadhi ya masuala hayo. Moja ya sifa kubwa ambayo Mwasisi wa Taifa hili Hayati Mwalimu Nyerere aliyotuachia ni kuweka misimamo kwenye misingi tunayoiamini kama Taifa. Kutokana na hali hiyo, Tanzania kama nchi huru imeweza kuwa na misimamo yake kuhusiana na masuala hayo kama yanavyoelezewa hapa chini.

Suala la Mpaka Kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa
Mheshimiwa Spika, lipo tatizo la muda mrefu kati yetu na nchi jirani ya Malawi linalohusiana na mpaka kwenye Ziwa Nyasa. Tatizo lenyewe ni kwamba Malawi wanadai kuwa Ziwa lote Kaskazini ya Msumbiji kuelekea Ruvuma na Mbeya ni mali yao kwa mujibu wa Mkataba wa Heligoland uliowekwa saini tarehe 1 Julai 1890.

Mheshimiwa Spika, Tanzania kwa upande wetu tunasema kuwa mpaka wa kweli kati yetu na Malawi unapita katikati ya Ziwa hivyo kufanya eneo lote la kaskazini mashariki ya Ziwa kati ya Latitude digree 9° na digree 11° kuwa mali ya Tanzania kwa mujibu wa Mkataba huo huo wa Heligoland (Ango-German Agreement) wa mwaka 1890 ambao ulikubali kuwa kwa vile kuna maeneo ya mpaka ambayo hayana mantiki, pande zinazohusika zikutane na kurekebisha kwa kuunda “Border Commissions”. Aidha, tunazo ramani ambazo Waingereza wenyewe (ambao wakati huo walikuwa wakitawala Nyasaland na Tanganyika) walikubaliana kurekebisha na hivyo kusogeza mpaka katikati kama ulivyo mpaka kati ya Malawi na Msumbiji.


Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo hili, mwaka 2005 Marehemu Rais Bingu wa Mutharika, alimwandikia Rais wa awamu ya tatu Mheshimiwa Mkapa akimtaka waunde Kamati ya kuliangalia tatizo hilo na kulipatia ufumbuzi. Awamu ya Nne ikaendeleza kwa kuunda Kamati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje kuliangalia tatizo na kulitolea mapendekezo. Kama zilivyokutana mwaka 2010, mwaka 2012 zilikutana tena ili kuendeleza mazungumzo ya mwaka 2010 na pia kujadili matukio ya kuonekana kwa ndege ndogo ndogo za utafiti wa mafuta na gesi kwenye Ziwa Nyasa zikitafiti hadi pwani ya Ziwa hilo upande wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, baada ya majadiliano makubwa kati yetu na Malawi, Serikali yetu iliwataka wenzetu wa Serikali ya Malawi pamoja na kampuni za utafiti au uchimbaji kusitisha mara moja shughuli zote za utafiti hadi majadiliano yatakapokamilika. Ni matumaini yetu kuwa wenzetu wa Malawi wametuelewa. Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa mgogoro huu mbele ya safari kutatuliwa na Msuluhishi badala ya sisi wenyewe.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili ya mgogoro bado iko mezani kwa majadiliano. Kufuatia maelekezo ya Marais wa pande mbili, Mawaziri wa Mambo ya Nje na wataalamu wetu wa masuala ya mipaka, ulinzi na usalama tulikutana Dar es Salaam tarehe 27 Julai, 2012 kujadili kwa kina mgogoro na kuupatia suluhu ya kudumu. Majadiliano yanaendelea vizuri na tumekubaliana kuwa wakati tukiendelea na mazungumzo, nchi zote zijiepushe na shughuli zozote kwenye Ziwa Nyasa ambazo zinaweza kutafsiriwa kuathiri maslahi ya nchi mojawapo. Kwa makubaliano haya, naomba niwatoe hofu wananchi wa mikoa ya Mbeya na Ruvuma kuhusu hali ya usalama mpakani mwa nchi yetu na Malawi. Chini ya uongozi wa Serikali ya CCM, wananchi wa Tanzania daima watakuwa salama dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho la kiusalama. Tumefanya hivyo tokea uhuru na hatutachelea kufanya vinginevyo wakati wote tukiwa madarakani. Hili limeelezewa katika Ibara ya Nane, aya ya 191 na 192 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 - 2015.

No comments:

Post a Comment