Kambi rasmi ya Upinzania Bungeni imeibua tuhuma nzito za kuwepo taarifa za baadhi ya watumishi wa Serikali kuhusika katika matukio ya ujangili katika hifadhi za taifa. Tuhuma hizo ziliibuliwa jana na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Mchungaji Peter Msigwa wakati akiwasilisha makadilio na matumizi ya bajeti ya kambi ya upinzani katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Alisema kuwa hali hiyo inasababishwa na taarifa za uchunguzi kuzifikia mamlaka za Serikali pasipo kuzifanyia kazi huku watumishi hawa ambao ni askari polisi wakitumia magari ya Serikali na magari yao binafsi kusindikiza misafara iliyobeba mizigo ya nyara za Serikali.
"Kambi ya upinzani inashangazwa na ukimya wa Serikali pale uchunguzi unapothibitisha ushiriki wa baadhi ya watumishi katika ujangili, ambapo pamoja na wahusika kufahamika kwa majina bado kumekuwa na udhaifu na ulegelege katika kuwachukulia hatua,"alisema.
Mchungaji Msigwa alisema kuwa wanazo taarifa kuhusu kupewa dhamana kwenye Mahakama ya Serengeti, Mugumu mtuhumiwa aitwaye Bw.Bryson Baloshigwa Naftali, mkazi wa kijiji cha Busunzu, wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma ambaye anadaiwa ni kiongozi mkuu wa mtandao wa ufadhili wa uwindaji faru na biashara haramu ya meno ya tembo katika hifadhi za Serengeti,Katavi, Tarangire, Ziwa Manyara, Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Mapori ya Akiba kama Ugalla, Rungwe, Moyowosi, Maswa.
"Kambi Rasmi ya Upinzani ina taarifa na ushahidi kuwa nyara zinazopatikana huzisafirisha nje ya nchi kwenda Burundi, Uganda na kwingineko ambapo mtuhumiwa amejitengenezea mtandao mkubwa ulioenea hapa nchini,"alisema mchungaji huyo wakati akiwasilisha makadilio ya bajeti ya Wizara hiyo kwa kambi ya upinzani.
Alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Juni 11,2012 na kesi yake kupewa kumbukumbu namba MUG/IR/1330/2012 akiwa kwenye kituo cha Polisi cha Kibondo lakini baada ya kufikishwa Mugumu,alilegezewa masharti ambapo mtuhumiwa huyo pamoja na mwenzake,Bw.Kama Yohana Tika ambaye anadaiwa kuwa ni mpigaji Tembo maarufu mkoani Kigoma na mwakilishi mkuu wa Bw. Bryson katika ujangili walifunguliwa kesi tofauti na tuhuma zao.
Mchungaji Msigwa alisema kuwa kesi waliyofunguliwa watuhumiwa hao ni ya kuazimisha silaha ambayo ina urahisi wa kupata dhamana,na wengine kufunguliwa kesi ya ujambazi kutumia silaha kwa baadhi ya washirika wake wasio na ushawishi wa fedha.
Waziri Kivuli huyo alisema kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitishwa na utendaji wa mamlaka za serikali na serikali yenyewe,pamoja na kuwepo kwa taarifa hizo lakini Serikali imeendelea kuwaacha huru watuhumiwa hawa bila kuchukua hatua madhubuti na kuendelea na kuzimaliza maliasili za nchi hii.
"Ulegevu huu wa Serikali ukiambatana na mazingira ya rushwa ulithibitika mnamo Julai 9 mwaka huu ambapo mtuhumiwa Bryson alipochukuliwa rumande, kwa kibali maalum “removal order” na kufikishwa mahakamani kisha kupata dhamana,"alisema mchungaji huyo.
Alifafanua kuwa inavyosemekana mtuhumiwa alitarajiwa kurudishwa Kigoma kwa gharama za Serikali kama alivyoletwa hapo Mugumu kwa kusindikizwa na Polisi lakini badala yake akaachiwa kwa dhamana.
Alisema Kambi ya Upinzani, inaitaka Serikali kutoa majibu kama watuhumiwa wa ujangili wanafikishwa na kuondolewa pasipo kufuata taratibu za kisheria na kuwaachia huru na akasema kwamba huu ndio uthibitisho kwa Watanzania jinsi tulivyo na Serikali iliyojaa rushwa na yenye kufumbia macho vitendo vikubwa vya rushwa hivyo Watanzania kupoteza matumaini na kukosa imani na vyombo vyao vya dola hasa Jeshi la Polisi
No comments:
Post a Comment