Waziri wa
Uchukuzi Dk, Harson Mwakyembe, amesema Oktoba mwaka huu, wakazi wa Jiji la Dar
es Salaam, wataanza kutumia usafiri wa reli, alizungumza hayo jijini Dar es
Salaam baada ya kutembelea Karakana ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), pamoja
na kukagua maendeleo ya mradi wa usafiri
wa reli ndani ya Jiji.
Katika ziara hiyo, Mwakyembe aliagiza watu waliojenga ndani ya meta 15 kutoka katikati ya reli kuondoka mara moja, alisisitiza kuwa vinginevyo wakati ukifika, nyumba za maeneo hayo zitavunjwa kwa nguvu na kwamba wamiliki wake hawatalipwa fidia.
“Nitalipeleka swala hili bungeni kwa sababu nimeshuhudia wazi watu wakiwa wanaishi katika maeneo ambayo hayastahili,pamoja na hayo wengine wamefikia hatua ya kulima mazao mbalimbali karibu na reli, jambo ambalo ni la hatari kwa usalama wao,” alisema.
Alisema tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam litamalizika Oktoba mwaka huu baada ya kukamilika kwa ukarabari wa mabehewa na reli kutoka Ubungo Maziwa hadi Stesheni.
Dk Mwakyembe alisema Serikali imelazimika kutumia fedha za ndani kukarabati mabehewa na reli, ili kuharakisha mkakati wa kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
“Serikali imeamua kufanya matengenezo ya mabehewa na ukarabati wa reli kuanzia Ubungo Maziwa hadi Stesheni ili kupunguza kama si kumaliza kabisa tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaa na kuruhusu shughuli za kiuchumi kuchukua nafasi ,” alisema Dk Mwakyembe.
Alielezea matumaini yake kuwa kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi tatizo la msongamano wa magari litakwisha kabisa hasa kwa kuzingatia kuwa kuna mradi wa magari yaendayo kasi.
Aliongezea kuwa ingawa Serikali inaendelea na jitihada hizo, lakini inakwazwa na tatizo la kukosekana kwa mali pa kuegeshea magari.
No comments:
Post a Comment