Wednesday, July 4, 2012

MVUTANO BUNGENI CCM, CHADEMA, CUF

'liwalo na liwe' *Mhagama apata wakati mgumu kutuliza malumbano bungeni *Nchemba ahusishwa na ufisadi, Mnyika atakiwa kuthibitisha

HALI si shwali ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ndivyo tunavyoweza kusema kutokana na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF), kurushiana makombora mazito.

Makombora hayo yaliibuka baada ya kuanza mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Katika mjadala huo, Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika (CHADEMA), alidai Bw. Mwigulu Nchemba (Mbunge wa Iramba Magharibi-CCM), ni miongoni mwa watuhumiwa wa wizi wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu (BoT).

Alisema inashangaza Idara ya Usalama wa Taifa kuzuia kashfa ya EPA isijadiliwe bungeni. Baada ya kupewa fursa ya kuchangia mjadala huo, Bw. Nchemba alipinda vikali madai hayo.

Aliongeza kuwa, kitendo cha kambi ya upinzani bungeni kuituhumu Idara ya Usalama wa Taifa kuwa imeshindwa kufanya kazi ya kuzuia ufisadi wa Fedha za Umma haina tija.

“Idara hii ni nyeti na haifanyi kazi za kuonekana kama askari wa usalama barabarani, lini idara hii ilihusika kukwamisha taarifa za ufisadi, Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza yale yaliyotokea BoT mwaka 2004-2005, mimi nilikuwa Chuo Kikuu.

“Nilijiunga na BoT, Oktoba mosi 2006, wakati wizi huu unatokea hata mlango wa Benki Kuu nilikuwa siujui,” alisema Bw. Nchemba.

Katika maelezo yake bungeni, Bw. Mnyika alisisitiza Bw. Nchemba alihusika na ufisadi wa fedha hizo. “Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkutano wa tisa wa Bunge, tulileta ushahidi wa barua ya Usalama wa Taifa kwenye kashfa ya EPA.

“Idara hii ilitoa agizo la kuzuia jambo hili lisijadiliwe bungeni na ushahidi huu upo katika kumbukumbu za Bunge,” alisema.

Baada ya kutoa tuhuma hizo, Mwenyekiti wa Bunge Bi. Jenister Mhagama, alitoa siku saba kwa Bw. Mnyika kuthibitisha namna Bw. Nchemba alivyohusika na ufisadi wa fedha za EPA.

“Nakupa siku saba uwe umethibitisha tuhuma zako hapa bungeni, tuhuma hizi zinamgusa moja kwa moja Bw. Nchemba,” alisema Bi. Mhagamal.

Baada ya Bi. Mhagama kutoa maelekezo hayo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. George Simbachawene ambaye kabla hajateuliwa katika nafasi hiyo alikuwa Mwenyekiti wa Bunge, alisimama na kudai wabunge wanakiuka kanuni zilizopo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni za Bunge zinavunjwa sana,...nini kinaweza kusaidia bunge lako kwenda vizuri, ningekuomba sana suala la miongozo, taarifa linatumia muda wa wachangiaji wengine ambao wangeweza kuisaidia Serikali.

“Kanuni haziruhusu mtu kulisemea jambo moja zaidi ya mara moja, mbunge anaposimama mara kwa mara anachosha watazamaji na bunge lako linashuka kiwango, watu wamechoka na vituko vya humu ndani,” alisema Bw. Simbachawene.

Wakati akiendelea kuchangia mjadala baada ya Bw. Simbachawene kutoa ufaafanuzi huo, Bw. Nchemba alidai kuhuzunishwa na hotuba ya kambi ya upinzani kuwalaumu walimu wa shule za msingi ambao hufanya biashara shuleni wakati wa masomo.

“Kauli hii ni fedheha kubwa kwa walimu ambao mimi binafsi naweaheshimu sana kutokana na mchango wao kwa maendeleo ya Taifa jili kwa sababu si wote wanaofanya biashara kama hotuba hii inavyosema,” alisema Bw. Nchemba.

Mbunge wa Viti Maalumu Bi. Sabreena Sungura (CHADEMA), aliomba mwongozo wa Mwenyekiti na kudai kuwa, taarifa hiyo haijasema walimu wote isipokuwa baadhi ambao ndio hufanya biashara na kama anataka ushahidi watampa.

Kutokana na hali hiyo, Bw. Nchemba alisimama tena na kusisitiza kuwa; “Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ninachosema kipo katika hotuba yao, mbunge aliyemaliza kusema hivi sasa (Bi. Sungura), labda arudi darasa la kwanza akafundishwe kusoma,” alisema.

Wakati huo huo, akihitimisha bajeti ya Wizara yake bungeni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Celina Kombani, alisema mwaka hu Serikali ilitenga sh. bilioni 10 kwa viongozi wakuu wastaafu nchini kwa ajili ya matibabu yao.

Alisema viongozi hao ni marais wastaafu na Mawaziri Wakuu wastaafu ambapo Bw. Augustino Mrema, hayupo katika orodha ya viongozi hao kutokana na nafasi aliyokuwa nayo serikalini kutotambuliwa kikatiba.

Kwa mara nyingine, Bi. Kombani alishindwa kutangaza kima cha chini cha mshahara wa watumishi wa umma na kusisitiza kuwa, watumishi wanaotaka kujua kima cha mshahara wao wakaulize katika vyama vyao vya wafanyakazi.

“Pendekezo la kutaka kima cha chini sh. 315,000, haliwezekani kutekelezwa kwa sasa kwani Serikali inahitaji kuwa na bajeti ya sh. trilioni 6.9 kwa ajili ya mishahara pekee,” alisema.

No comments:

Post a Comment