*Wauguzi wakosa kazi, RC Dar atoa tathmini
Madaktari hao wameapa kuwa, hawataingia kazini hadi madaktari waliopo kwenye mafunzo ya vitendo waliopewa barua za kurejeshwa wizarani watakaporudishwa kazini.
Kutokana na mgomo huo, baadhi ya wauguzi hospitalini hapo, jana walionekana wakiwa wamelala katika mabenchi na wengine wakiwa katika vikundi wakijadili mambo mbalimbali.
Baadhi ya wauguzi waliozungumza na Majira, wamelalamikia hali ya kipato chao hasa kipindi hiki cha mgomo hivyo kudhihirisha kuwa, kabla ya mgomo wauguzi hao walikuwa wakinufaika.
Madaktari Bingwa katika hospitali hiyo, walitangaza kuanza mgomo huo siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuhutubia Taifa na kutangaza msimamo wa Serikali kuwa haina uwezo wa kuwalipa mshahara wanaotaka.
Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete alisema daktari ambaye haridhiki na mshahara anaopata, aache kazi na kwenda kwa mwajiri ambaye atakuwa na uwezo wa kumlipa mshahara anaotaka.
Madaktari hao, wameweka wazi kuwa bila wasaidizi wao, hawawezi kuendelea kutoa huduma za matibabu ambapo mgomo huo umechangia baadhi ya wagojwa kuondoka hospitalini.
Katibu wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dkt. Edwin Chitage, alisema madai yao si ya mshahara na posho kama inavyoelezwa na Serikali bali ni pamoja na kutaka waboreshewe mazingira ya kazi sambamba na kupatiwa vitendea kazi.
“Tuna madai mengi lakini nashangaa hotuba ya mkuu wa nchi, haikuzungumza dai lolote la ukosefu wa vitendea kazi katika hospitali zilizopo nchini zikiwemo za Wilaya,” alisema.
Katika hatua nyingine, Hospitali ya Ocean Road ambayo inatoa matibabu kwa wagojwa ya saratani, hali ya huduma jana ilizidi kusuasua huku wagonjwa wakilalamika kukosa matibabu.
Wakizungumza na Majira kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, baadhi ya wagonjwa walisema hakuna huduma walizopata tangu jana asubuhi hivyo kusababisha msongamano hospitalini hapo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala Dkt. Sophincas Ngonyani, alikanusha madai ya kuwepo daktari aliyetekwa katika hospitali hiyo.
“Jana (juzi) walikuja polisi kufuatilia suala hili lakini hakuna tukio kama hilo ni uzushi mtupu,” alisema.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Meck Sadick, amesema hali ya utoaji huduma katika hopitali za Amana, Temeke na Mwananyamala, imeimarika ingawa kuna upungufu wa madaktari 66 ambao wanashiriki mgomo huo.
Alisema huduma katika hospitali hizo zinaendelea kama kawaida baada ya kufanya ziara akiwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kufanya ziara maalumu.
Aliongeza kuwa, katika Hospitali ya Amana Daktari Bingwa mmoja ambaye ambaye hakuwepo kazini lakini katika hospitali za Temeke na Mwananyamala, walikuwepo.
Alitoa mwito kwa wananchi kwenda katika hospitali hizo kupata huduma na kuwa, kitengo cha dharura kitaimarishwa kwa ajili ya kupokea wagonjwa.
source:majira.co.tz
No comments:
Post a Comment