Shirika la Kimataifa linaloshughulikia wakimbizi duniani UNHCR limeipongeza serikali ya Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kupokea wakimbizi wanaotoka nchi mbalimbali za Afrika na kuwapatia makazi pamoja na usalama.
Hayo yalisemwa na Mwakilishi wa UNHCR Bi.Chansa Kapaya wakati wa maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa juzi jijini Dar es Salaam.
Katika maadhimisho hayo Bi. Chansa alisema kuwa kwa miongo minne sasa serikali ya Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuwapokea na kuwasaidia wakimbizi kwa kuwapatia makazi.
"Kwa mfano mwaka 2010 serikali ya Tanzania ilitoa idhini ya kuruhusu wakimbizi 162,000 wa kutoka Burundi kupatiwa uraia wakudumu ambao waliishi kwa muda wa miaka 40 kwenye kambi mbalimbali za wakimbizi nchini", alisema.
Mbali na hayo alisema kuwa kwa miaka ya hivi karibuni idadi ya wakimbizi walio katika kambi mbalimbali za wakimbizi nchini imepungua kwani wengi wao wamefanikiwa kurudishwa makwao.
Alisema zaidi ya wakimbizi laki 5 wamefanikiwa kurudishwa makwao na wengine tayari wamepatiwa uraia wa kudumu nchini.
Wakimbizi wanalazimika kuhama nchini mwao kwenda sehemu nyingine duniani kwa ajili ya kutafuta makazi na usalama kutokana na machafuko yaliyo tokea na yanayo endelea kutokea nchini mwao.
Ripoti iliyotolewa na Shirika hilo ya mwaka 2011 inaonesha kuwa watu laki 8 wanalazimika kuhama nchi zao huku Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiwa ni miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kuzalisha wakimbizi duniani.
Naye Bw. Walter Bgoya Mchapishaji katika Kampuni ya Mkuki na Nyota alisema japokuwa wakimbizi wanapata changamoto nyingi katika kambi zao lakini serikali ya Tanzania inawajibu wa kupewa shukrani za dhati kwa kuwa tayari kujitolea kuwapokea wakimbizi na kuwapatia haki zao za msingi kama vile usalama.
Kwa upande mwingine ujumbe uliotoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki- moon ulisema kuwa tunawajibu wa kufanya kazi kwa pamoja ili kuwahamasisha viongozi wa siasa kuzuia migogoro ambayo itasababisha machafuko nchini mwao.
Aidha ujumbe huo ulisema kuwa wapiganaji wote duniani waweke silaha zao chini na kutafuta suluhisho la migogoro yao kwa amani ili kuzuia kuongezeka kwa wakimbizi duniani.
Siku ya wakimbizi duniani huadhimishwa kila ifikapo Juni 20 ya kila mwaka amabapo lengo lake kubwa ni kuwaunganisha wakimbizi wote kuwa pamoja na kujiona kuwa wako sawa na raia wa kawaida.
No comments:
Post a Comment