CHAMA cha kuogelea Tanzania (TSA) kimewataka wanachama wake 13 kuandaa mafunzo ya kuogelea na uokoaji kama yaliyofanywa na Klabu ya Tanzania Marine Swiming Clab (TMSC) ili kuwasaidia watanzania wengi kupata mbinu ya kujiokoa.
Akizungumza Dar es Salaam juzi wakati wa kufungwa kwa mafunzo ya kuogelea na uokoaji yaliyofanywa na TMSC Katibu Mkuu wa TSA, Noel Kiunsi alisema hii ni mara ya kwanza klwa mwanachama wa TSA kuandaa mafunzo hayo ambayo kwa kiasi kikubwa pia yanasaidia kuutangaza mchezo huo.
Alisema TSA imeanzisha programu ya kuendeleza mafunzo ya uokoaji chini ya Baraza la Michezo Taifa (BMT) ambapo kwa sasa wapo katika mchakato wa kupata fedha kwa ajili ya kuanza programu hiyo ambayo itakuwa ikiendeshwa na TSA pamoja na wanachama wake ambao ni klabu kwa nchi nzima.
Alisema msukumo wa kuanzisha programu hiyo umetokana na matukio endelevu yanayotokea majini hasa katika vyombo vya usafiri huku akizitaja ajali za majini ambazo ziliwahi kupoteza maisha ya watu wengi kama ajali ya Meli ya MV Bukoba na ile ya MV Spice Islander.
Alisema endapo watanzania wengi watapatiwa mafunzo hayo kutaepusha wimbi la watu kuzama majini hasa yanapotokea majanga katika vyombo vya usafiri na hata vile vya angani ambavyo hukimbilia baharini kwa kunusuru maisha yao.
Kiunsi alitaja wanachama wao ambao watashirikiana katika kuendesha programu hiyo ni Talis, Hopac, UDSM, TMSC, Dar swim, Stringleis, Isamilo, Agakhan, JKT na klabu za Zanzibar.
No comments:
Post a Comment