TATIZO la bidhaa feki zisizokidhi viwango nchini Tanzania huathiri uchumi wa Taifa kwa namna mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuikosesha serikali mapato pamoja na kupunguza ajira za wananchi kutokana na kuvikosesha viwanda vya nchini fursa ya kukua na kuajiri na kuipatia serikali mapato.
Hali hii pia husababisha wawekezaji kuogopa kuja kuwekeza nchini, kwani bidhaa duni hutishia afya na usalama wa umma na kuharibu mazingira.
Uzoefu unaonesha kuwa baadhi ya nchi zilizioendelea zimefanikiwa kulinda masoko yao ya ndani dhidi ya bidhaa duni kwa kutekeleza mpango wa (PVOC ) wa kukagua na kudhibiti ubora wa bidhaa katika nchi zinakotokana kabla hazijasafirishwa kuja nchini.
Mfumo huu wa kukagua na kudhibiti bidhaa unaweza kufanikiwa hata kwa Tanzania na kulinda soko la Tanzania dhidi ya bidhaa duni na bandia zinazoingizwa katika nchi mbali mbali.
Akizungumza hivi karibuni katika mkutano wa Mawakala wa Forodha Tanzania Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania(TBS)Bw.Leandri Kinabo, anasema kuwa kwa kutumia Mpango huo wa kukagua na kudhibiti ubora wa bidhaa katika nchi zinakotoka kabla hazijasafirishwa Tanzania inaweza kupiga hatua .
Anasema kuwa lazima kuweka msisitizo kuhusiana na umuhimu wa kulinda soko la Tanzania dhidi ya bidhaa duni na bandia zinazoingizwa kutoka nchi mbali mbali.
Anasema kuwa licha ya jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na taasisi mbali mbali ikiwamo Tbs katika kusimamia ubora na usalama wa bidhaa zinazoingia nchini bado nchi haijaweza kufanikiwa kumaliza tatizo la bidhaa hafifu na bandia sokoni.
Anaelezea kuwa Mfumo huu wa udhibiti umefanikiwa kupunguza kiasi cha bidha duni zinazoingizwa nchini, hata hivyo haujaweza kufanikiwa kwa asilimia 100 kuilinda nchi dhidi ya bidhaa duni na bandia hivyo kuwepo kwa haja ya kuchukua hatua za ziada kwa ajili ya kulinda nchi yetu isiwe jalala la bidhaa zisizofaa kwa matumizi.
Naye Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa ViwangoTanzania Bi Kezia Mbwambo anasema kuwa PVOC ni mpango wa kudhibitri ubora ambao hutumika kuthibitisha kuwa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nchi mbali mbali zinazokidhi matakwa ya viwango kabla ya kusafirishwa kwenda katika nchi husika.
Anasema kuwa madhumuni ya mpango huo nchini Tanzania ni kuhakikisha kuwa bidhaa zote zinakidhi matakwa ya viwango husika kabla ya kusafirishwa kuja nchini,kulinda afya ya umma usalama wa walaji na mazingira, kuleta ufanisi katika kuondoa bidhaa bandarini hivyo kurahisisha biashara pamoja na kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani usio sawa na bidhaa zisizofaa.
Bi.Mbwambo anasema kuwa pamoja na kutumia mfumo huo wanakabiliwa na changamoto ya kushindwa kudhibiti kwa asilimia 100 bidhaa zinazoingia kutokana na njia nyingi za kuingilia zikiwamo zisizo rasmi.
Pia anaelezea kuwa ugumu katika kushughulikia bidhaa duni zinazoingizwa nchini kuzirudisha zinakotoka au kuziharibu, uhaba wa mahali pa kuhifadhia shehena za bidhaa duni TPAna TRA, ugumu wa kuthibitisha ubora wa baadhi ya bidhaa pamoja na ucheleweshaji unaotokana na taratibu za udhibiti.
Anasema kuwa kwa kutumia mpango huo kuna njia kuu mbili za ukaguzi ukaguzi wa bidhaa zikiwa tayari kwenye bandari husika na ukaguzi wa bidhaa katika nchi zinakotoka kabla haijasafirishwa kwenda kwenye nchi zinakokwenda.
Kutokana na ugumu uliojitokeza katika utekelezaji waTBS ilimua kutafuta hatua za ziada za udhibiti wa bidhaa zinazotokana nje kwa lengo la kupunguza na kuondoa ugumu uliopo sasa, kupata ufanisi zaidi.
Akizungumzia hivi karibuni Rais wa Chama cha Wakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) Bw. Steven Ngatunga anasema kuwa ili kudhibiti ubora wa bidhaa feki lazima Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kushirikina na Kampuni zilizoshinda zabuni kwenda kukagua bidhaa viwandani kabla hazijasafirishwa kuja hapa nchini.
Anasema kuwa bila kuchukua hatua za kwenda kukagua viwandani Tanzania itaendelea kuwa na bidhaa feki na kuchangia kudorora kwa uchumi wa Tanzania
No comments:
Post a Comment