Wednesday, June 27, 2012
MAT WALAANI KITENDO CHA KUPIGWA KWA DKT ULIMBOKA
Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimelaani kitendo cha kupigwa kwa
mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dkt.Steven Ulimboka kimewavunja mioyo na kuondoa huruma na unyenyekevu kwa watumishi.
Akizungumza Dar es Salaam na waandishi wa habari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Rais wa MAT Dkt. Lamara Mkopi alisema kuwa wanalaani kitendo hicho ambacho kimewafedhehesha watumishi wa sekta ya afya nchini.
Dkt.Mkopi alisema MAT ni chama cha kulinda, kutetea maslahi ya madaktari pamoja na wafanyakazi wa sekta ya afya na majukumu mengine ni kuangalia mustakabali mzima wa sekta ya afya kwa maslahi ya wananchi.
Alisema kuwa MAT ilipata taarifa juzi za kutekwa kwa kiongozi huyo mbele ya watumishi wa Serikali (akimaanisha Ikulu) kuwa daktari huyo alitekwa na watu watano wenye silaha baada ya kuitwa na mtu mmoja.
Alisema kuwa baada ya kuwepo kwa taarifa hizo walitoa taarifa polisi lakini cha kusikitisha walikataa kufahamu taarifa hizo.
Alisema asubuhi kwa bahati nzuri ama mbaya kwa wahusika waliofanya kitendo hicho Dkt.Ulimboka alikutwa Mabwepande akiwa hai na kupelekwa katika kituo cha polisi Bunju.
"Pamoja na kufikishwa kituoni hapo polisi walishindwa kumpeleka hospitali na juhudi za kutafuta gari la kubebea wagonjwa la Muhimbili ilishindikana, " alisema.
Kwa upande wa Jumuiya ya Madaktari, imesema kuwa kutokana na tukio hilo limewapa nguvu zaidi ya kuendelea kudai madai yao hata kwa kutoa uhai wao.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo katibu wa jumuiya hiyo Dkt.Edwin Chitage, alisema kuwa jumuiya hiyo itasimama imara hata kwa gharama zozote.
Pia alisema kuwa ni bora madaktari na watumishi wote kulaani kitendo hicho ni kitendo cha kidhalimu na kulaaniwa si kwa madaktari tu bali hata kwa Watanzania wanaoitakia amani nchi.
Aliongeza kuwa wanalaani wale wote waliosababisha kucheleweshwa kwa Dkt. Ulimboka kufikishwa hospitalini na hata hivyo wanamshukuru Mungu kwa kuwa anaendelea na matibabu.
"Tunaishukuru AAR kwa kutoa gari ambapo Muhimbili iligonga mwamba hivyo madaktari tunawasii kuendelea kusimama imara na kuendelea kudai haki zao licha ya kuwepo kwa juhudi za watu za kuhakikisha lengo lao litimie kwa nia ya kuondoa uhai wake, " alisema.
Hata hivyo Taasisi za Kutetea Haki za binadamu, imeiomba Serikali kufanya uchunguzi wa kimataifa ili kuweza kuwabaini wahusika.
Akizungumza na waandishi wa habari mkugenzi wa shirika liliso la kiserikali la SIKIKA na kwa niaba ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Bw.Erinei Kiria, alisema Dkt. Ulimboka alikuwa kiongozi wa mgomo wa madaktari.
Alisema kitendo cha kutekwa na kuokotwa jana asubuhi huku akiwa amepigwa vibaya na kunyang'anywa nguo zake ni cha kinyama na uharamia.
Alisema kuwa kitendo hicho hakistahili kutendwa kwa binadamu yeyote haiwezekani binadamu kupigwa na kuumizwa kwa namna hiyo hiki ni kinyume na haki za binadamu.
Alisema kuwa jana asubuhi alishuhudia Waziri Pinda akisema bungeni kwa kumalizia kuwa 'Serikali itachukua hatua na liwalo na liwe' alisema kwa kauli hiyo wanasikitika imetoka kwa kiongozi mkuu.
Pia kauli hiyo ameizungumza kwenye chombo kitukufu kama Bunge na spika hakuchukua tahadhari kwa kusahahisha wala kupata ufafanuzi kwa kauli hiyo.
Alisema ingawa hawana ushahidi na hawajui hivyo wanajiuliza kama 'liwalo liwe' kama limeanza kwa Dkt. Ulimboka kupigwa hivyo wana hofu ya Serikali kuwapeleka pabaya na haina nia njema na Watanzania.
Alisema kuwa wanaharakati wanagombea haki za madaktari kwa kuwa Serikali ina orodha ya madai yao na hatua hiyo inatokana na Serikali kushindwa kuwatimizia madai yao.
Alisema madaktari wanafanyakazi katika mazingira magumu kutokana na kutokuwepo kwa vifaa, dawa lakini vitendo hivyo vimekuwa havijadiliki.
"Tuna imani kuwa kama madaktari wakipata huduma nzuri hata suala la afya litaboreshwa na kuondokana na malalamiko ya wananchi kukosa dawa kwenye hospitali, " alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Bi. Hellen Kijo Bisimba alisema ni bora Serikali ikaunda tume huru itakayochunguza suala hilo hata kama itakuwa ni tume huru ambayo itaweza kusaidia kuwa kama hawahukusika na tukio hilo.
Labels:
Habari
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment