Monday, June 25, 2012

CUF WATAKA OFISI YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA ICHUNGUZWE

Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kauli aliyotoa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Bw. John Tendwa, kuwa atavifuta baadhi ya vyama vya mifukoni, inaudhi na kusikitisha hivyo ofisi yake inapaswa kuchunguzwa.


Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Naibu Katibu Mkuu wa CUB Bara, Bw. Julius Mtatiro, ili sema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, ofisi hiyo ndiyo yenye dhamana ya kusajili vyama husika vya siasa.

Alisema Bw. Tendwa alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika hafla ya kukabidhi cheti cha usajili wa kudumu kwa Chama cha Kijamii (CCK).

Aliongeza kuwa, uwepo wa vyama vya mifukoni unachangiwa na Bw. Tendwa hivyo kauli yake ya kutaka kuvifuta haina tija kwa sababu haitekelezeki.

“Nchi yetu imefikia mahali ambako watumishi ambao tumewakabidhi ofisi za umma, wanatudanganya hadharani na kuficha maovu ya ofisi za umma.

“Bw. Tendwa anahusika moja kwa moja kuhakikisha vyama dhaifu visivyo na vigezo vinasajiliwa, mkakati huu unafanywa ili kuweka utitiri wa vyama ambao hugeuka kuwa mawakala wa kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika chaguzi,” alisema.

Aliongeza kuwa, ukweli huo ulijionesha katika Uchaguzi Mkuu
mwaka 2010 ambapo baadhi ya vyama vya siasa, vilitangaza wazi kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete na kuzunguka nchi nzima kumpigia kampeni.

“Leo hii Bw. Tendwa anawahadaa Watanzania kuwa atavifuta vyama hivi, huu ni uzushi na uongo mkubwa, hawezi kuvifuta vyama dhaifu ambavyo amevisajili yeye mwenyewe ili kutekeleza mkakati wa kuisaidia CCM,” alisema Bw. Mtatiro.

Alisema CUF inataka Ofisi ya Msajili ichunguzwe kutokana na mashaka makubwa yaliyopo na viashiria vya ufisadi katika usajili wa baadhi ya vyama vya mifukoni.

“Taasii ya Kuzuia na Kupambgana na Rushwa (TAKUKURU), iwajibike kuichunguza ofisi hii na Bunge lifuatilie suala hili,” alisema..

No comments:

Post a Comment