WAFANYAKAZI wawili wa Benki ya Barclays na
mfanyabiashara mmoja, jana wamepandishwa kortini katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa kosa la kula njama na kuiba dola
za Marekani 34,000.
Washtakiwa hao ni Bw. Wilscate Ushiwe (20), Bw. Ramadhani Wagole (35) na mfanyabiahara Bw. Desire Mangongo (39).
Mbele
ya Hakimu Bw. Faisal Kahamba, wakili wa Serikali Bi. Willa Haoga,
alidai katika tarehe zisizofahamika mwaka huu jijini Dar es Salaam,
washtakiwa walikula njama ya kutenda makosa hayo.
Katika kosa la
kwanza, ilidaiwa Januari 14 mwaka huu wakiwa katika benki hiyo iliyopo
eneo la Slipway Msasani, wilayani Kinondoni, washtakiwa waliiba dola za
Marekani 9,000 kutoka akaunti namba 0127000379 ya Bw. Mohamed Salehe.
Shtaka
la pili, inadaiwa Januari 20 mwaka huu, washtakiwa waliiba dola za
Marekani 12,000 kutoka akaunti namba 0127020379 ya Bw. Mohamed Salehe.
Katika
shtaka la tatu, inadaiwa Januari 25 mwaka huu, washtakiwa waliiba dola
za Marekani 13,000 kutoka akaunti namba 0127020379 ya Bw. Mohamed
Salehe.
Washtakiwa wote walikana kutenda makosa hayo ambapo upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi haujakamilika.
Hakimu
Bw. Kahamba alidai washtakiwa wanaweza kuwa nje kwa dhamana kama
watatimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini hati ya
dhamana ya sh. milioni 10 kila mmoja.
Vigezo vingine ni kila
mshtakiwa kuwasilisha mahakamani sh. milioni 10 taslimu au hati ya mali
isiyohamishika yenye thamani hiyo. Washtakiwa wote walishindwa kutimiza
masharti hayo na kurudishwa rumande. Kesi imehairishwa hadi Julai 18
mwaka huu.
source: majira.co.tz
No comments:
Post a Comment