Wednesday, June 20, 2012

MAONI YA MUUNGANO KUWA HURU -TUME YA KATIBA

Tume ya kuratibu Maoni ya Katiba Mpya imesema haipo tayari kufanya kazi kwa kuingiliwa na mtu yeyote pamoja na kuwataka wananchi wajiandae kutoa maoni hayo bila woga.Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya katiba mpya Jaji Joseph Warioba mara baada ya kuulizwa swali kwa wakati wa kukusanya maoni ya wananchi Suala la Muungano lisijadiliwe pamoja na mtazamo wa kikundi cha uamsho ambacho kinadai serikali tatu.


"Tume iko tayari kukusanya maoni ya kila mtu awe anataka serikali moja mbili tatu , muungano uvunjwe watakusanya maoni yote na kuja kuyachambua ili tuweze kupata katiba ambayo inahitajika na wananchi,"alisema Jaji Warioba.

Alisema kuwa tume hiyo kwa sasa iko tayari kuanza kazi kwa awamu ya kwanza ya kukusanya na kuratibu maoni ya wananchi baada ya kufanya maandalizi ya kutosha ya kuandaa nyaraka muhimu kwa ajili ya kuwapatia wananchi elimu ya kutosha.

Alisema kuwa nyaraka hizo ni nakala laki tano za katiba ya Jamhuri ya muungano ya mwaka 1997 nakala elfu kumi za katiba ya Zanzibar, nakala laki tano ya sheria ya mabadiliko ya katiba ya 2012, tume kwa kutambua kwamba nyaraka hizo hazitoshi na hata kama zikipatikana kwa wingi ni vigumu kwa wananchi kuzisoma na kuzielewa kwa urahis wameandaa kwa lugha nyepesi.

"Tume imeandaa nyaraka ambazo ni rahisi kuzisoma na kuzielewa ambayo ni katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania , sheria ya mabadiliko ya katiba ya 2012 kwa lugha nyepesi, hadidu za rejea, programu ya elimu kwa Umma,"alisema.

Alisema kuwa tume hiyo itaanza safari za mikoani na imejigawa katika makundi saba na kila kundi litafanya safari nne mikoani kati ya sasa na mwisho wa mwaka na kila kundi litafanya kazi kwa wastani wa mwezi mmoja kila mkoa isipokuwa kwenye mikoa midogo

Alisema kuwa wataanza na Mikoa nane ya Dodoma, Kagera ,Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara ,Pwani Shinyanga na Tanga hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao kwa uwazi bila ya hofu yoyote na kwa utulivu, wawe wavumilivu na watoe maoni bila jazba au kubeza.

Jaji Warioba alisema kuwa tume kwa kiwango fulani imeanza kuratibu maoni ya wananchi na kuona mwelekeo na kubaini maeneo ya kufanyia kazi unaanza kuonekana hasa kuhusu taasisi za dola kama serikali na vyombo vyake vyote, tume inaomba maeneo mengine nayo yapewe uzito hasa yaliyo katika sura ya kwanza ya katiba kwani sehemu hiyo ni moyo wa katiba.

Alisema kuwa eneo la kwanza ni Misingi ya Taifa, kwani ndiyo nguzo ya utamaduni wa wananchi wake, ndiyo nguzo ya nidhamu, maadili ya nchi na wananchi wake, kwani katiba ya sasa imetaja kuwa ni uhuru, Haki, undugu, Demokrasia na serikali kutofungamana na dini yoyote hivyo tume ingetaka kupata maoni ya wananchi kuhusu eneo hilo.

Alitaja maeneo mengine ni kuhusu mamlaka ya wananachi kwani katiba ya sasa inaelezea kwamba wananchi ndio msingi wa malaka yote, eneo la tatu ni malengo muhimu na misingi ya mwelekeo wa shughuli za serikali, eneo la nne ni haki za binadamu na wajibu kwa jamii.

Alisema kuwa kupitia maeneo hayo manne wananchi wanatakiwa kutoa maoni yao kwani malengo hayo ndiyo yanayojumuisha matumani ya Watanzania kuhusu aina ya Tanzania wanayoitaka, pia tume iweze kufahamu ndoto za wananchi kuhusu rasilimali za Taifa jinsi ya kuzilinda, kuziendeleza na kuzitumia .

Alisema kuwa awamu ya pili ya kukusanya maoni ya wananchi itafanyika kupitia mabaraza ya Katiba, hivyo wananchi wanatakiwa kufika kwa wingi katika mikutano ya ukusanyaji maoni katika awamu zote mbili na watoe maoni yao kwa uwazi bila ya hofu yoyote, na tume itafanya kazi kwa uwazi na maoni yote yatakayotolewa na wananchi, taasisi, asasi za kiraia na makundi mengine yataheshimiwa na kufanyiwa kazi ipasavyo.

Jaji Warioba alisema kuwa pamoja na mikutano kufanyika kutakuwepo na mfumo wa kupokea maoni ya Watanzania kutoka pande zote za ndani na nje ya nchi kupitia simu, barua pepe, mitandao ya kijamii, faceebook, twitter blog na kwa njia ya posta.






No comments:

Post a Comment