*Wahariri watoa tamko zito
Bw. Kubenea aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema ameshangazwa na kitendo cha Serikali kulifungia gazeti hilo kwani barua waliyopokea, haielezi wamefungiwa kwa kosa gani.
“Serikali inapaswa kuacha kutishia maisha ya raia wake kwa njia ya kuwaondoa katika biashara na kuwaomba wasomaji pamoja na wadau wa habari, wasimame pamoja kudai haki ya kutafuta na kusambaza habari,” alisema.
Aliongeza kuwa, Serikali imedhamiria kuwatesa wafanyakazi na watendaji wengine wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers inayochapisha gazeti hilo kwa njia ya kulifungia.
“Kufungiwa gazeti hili kunahatarisha maisha ya wafanyakazi, wachapishaji na wauzaji kwani wote, Serikali imeweka misha yao kiganjan,” alisema Bw. Kubenea.
Naye Wakili wa Kampuni hiyo Bw. Rugemeleza Nshala, alisema kampuni hiyo itachukua hatua stahiki baada ya bodi ya Kampuni hiyo kukaa na kujadili kwa kina.
Wakati huo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimelaani uamuzi wa Serikali kulifungia gazeti hilo kwa muda usiojulikana.
Kimesema hatua hiyo ni matumizi mabaya ya sheria ya magazeti pamoja na kwenda kinyume na utawala bora.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana kwenye vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Bw. John Mnyika, imeitaka Serikali kulifungulia gazeti hilo haraka iwekanavyo.
Bw. Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema tayari chama chake kimewasiliana na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na chama hicho kuchukua hatua za kibunge kuisimamia Serikali, kurekebisha udhaifu huo kama itakuwa inaheshimu uhuru wa habari na inazingatia masilahi ya taifa.
“CHADEMA inaitafsiri hatua ya Serikali ya kulifungia gazeti hili ni sawa na kufungia uhuru wa kusambaza habari, kupokea na kutoa maoni hivyo tunatoa mwito kwa wananchi na wadau wote wa habari kuungana pamoja kupinga hatua hii,” alisema Bw. Mnyika.
Alisema chama hicho kitaendelea kuchukua hatua za ziada kama Serikali haitasikiliza kauli za wadau wa habari juu ya suala hili.
source:gazeti la majira
No comments:
Post a Comment