Saturday, July 28, 2012

YANGA BINGWA - KOMBE LA KAGAME


Timu ya Yanga ya Tanzania imefanikiwa kulitwaa tena kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati baada ya kuifunga timu ngeni kwenye mashindano hayo, Azam, kwa 2-0 Jumamosi, mjini Dar es Salaam.
Mshambuliaji wa kimataifa kutoka Uganda Hamis Kiiza alifunga bao la kwanza dakika ya 44 na Said Bahanuzi akaongeza kipindi cha dakika za nyongeza kuhakikisha Yanga wanalitetea kombe hilo.

Yanga wamezawadiwa dola 30,000, Azam wao wamepata dola 20,000 na Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo walioifunga APR ya Rwanda 2-1 kwenye mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu, wameondoka na dola 10,000.

Fedha hizo zimetolewa na Rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye ni mdhamini wa michuano hiyo kwa miaka zaidi ya 10 na mashindano hayo yamepewa jina lake.

Baada ya mchezo nahodha wa Yanga Nadir Haroub alimsifu kocha wao mpya kutoka Ubeligiji Tom Saintfield kwa maelekezo mazuri.

“Tumecheza vizuri na kwa kujituma ndio maana tumeshinda, tunae kocha mzuri na tumefuata maelekezo yake, ndio siri ya ushindi.

Naye kocha wa Azam kutoka Uingereza Stuart Hall alisema wamepata uzoefu licha ya kushindwa kutwaa kombe.

“Sasa Afrika nzima inajua uwezo wetu. Tuliwafunga Vita ya Congo na Tusker ya Kenya, na hii inaonyesha uwezo wetu,” alisema.




source:bbc swahili

No comments:

Post a Comment